Sunday, December 10, 2006

Prof. Ishengoma: Si lazima wote twende bungeni

Diwani msomi anayeongoza Kata ya Mbuyuni Morogoro
-Asema wanawake wasifungiwe kwenye chupa
-Vijana wengi wa Kitanzania awaita 'broilers'
na innocent munyuku
NI asubuhi ya saa mbili na nusu hivi. Jumamosi iliyotulia, siku ambayo nimejaa shauku ya kukutana na msomi aliyebobea katika masuala ya kilimo lakini akaamua kuwania nafasi ya chini katika siasa.
Huyu si mwingine bali ni Profesa Romanus Ishengoma (54), Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro ambaye hivi karibuni iliyopita amefanya mahojiano maalumu na RAI na kutoboa kisa cha yeye kujiingiza katika siasa akiwania nafasi ya chini kabisa.
Akiwa amevalia vazi la kaptula na shati la bluu ananifuata katika lango kuu la kuingilia nyumbani kwake eneo la Falkland mjini Morogoro. Ananikaribisha baada ya utambulisho mfupi. Ni mwingi wa mazungumzo lakini kila anachozungumza hasiti kukitolea mifano na wakati mwingine kukushirikisha katika mazungumzo kwa kuuliza maswali.
ÒUnaujua huu ni mti gani?Ó ananiuliza akinionyesha mti mmojawapo unaopendezesha nyumba yake iliyozungukwa na mti. Mti huo anaouliza ni wa aina ya cacao ambao kwa mazoea haulimwi nchini Tanzania.
Lakini baadaye ananieleza kuwa anaelewa fika kwamba si kwenda kuangalia miti aliyoipanda na hivyo ananipisha niendelee na kiini cha safari yangu.
Nami bila kusita namjibu kwamba kilichonileta ni habari ya miti pia kwa hiyo hana haja ya kuacha kuzungumzia suala la mazingira. Tunashirikiana kicheko na kuketi katika viti nje ya nyumba yake.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, wengi hawakuelewa pale waliposoma kwenye magazeti au kupata habari kupitia vyombo vingine kwamba Profesa wa Chuo Kikuu anawania nafasi ya udiwani wa Kata ya Mbuyuni mjini Morogoro.
Prof. Ishengoma analielezea jambo hilo kuwa ni msimamo wake katika maisha.
ÒSiwezi kuwa driven (kuendeshwa) na mkumbo, na hii ni kwa sababu nina elimu ambayo ndio msingi mkubwa wa maisha.
ÒKusema tu kwamba mimi ni profesa haitoshi, mchango wangu ni nini katika jamiiÉmaendeleo daima huanzia katika grass roots na huu ndio mchango,Ó anasema na kisha kuongeza:
ÒKwa hiyo unapozungumzia udiwani unazungumzia msingi wa mambo mengi ya jamii, na labda niwakumbushe wanaonishangaa kwamba udiwani hauniondelei uprofesa nilionao.Ó
Anasema aliona ni vema aanzie na udiwani kwani ipo haja ya kujenga msingi.
ÒNawashauri wasomi au niseme maprofesa wenzangu, tuache kulalamika na badala yake tuanze kuwaletea maendeleo wananchi sehemu tunazoishi.
ÒLakini hapa pia tuwekane sawa kwamba si lazima wote twende bungeni. Maprofesa wamebaki kulalamika na wengi hawataki kuwatumikia wananchi,Ó anasema.
Je, katika uchaguzi huo wa mwaka jana hakutengwa na wananchi wa Morogoro kwa ukabila hasa ikizingatiwa kwamba yeye ni mtu wa Bukoba?
ÒWananchi wa Morogoro si wakabila, naomba tusiwapakazie. Lakini niliwahi kusikia minongÕono juu ya jambo hilo. Lakini hawa mimi ni ndugu zangu.
ÒHili nalisema kwa uwazi kabisa, Waluguru ni ndugu zangu. Nimekaa hapa kwa miaka zaidi ya 30 na sioni kama natengwa kama wapo wenye hulka hiyo ni wachache. Sasa hatuwezi kusema Waluguru ni wakabila wakati wenye tabia hiyo si wengi.Ó
Anazungumziaje Serikali ya Rais Jakaya Kikwete hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwaka mmoja madarakani?
Prof. Ishengoma ambaye Januari 19 mwaka huu alichaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Morogoro anasema Kikwete kaanza vizuri katika uongozi wake.
ÒHuu mwaka mmoja wa Kikwete vya kusifiwa ni vingi kuliko lawama, kuna kasi ya maendeleoÉkuna attitude ya uwajibikaji kwa viongozi.
ÒAmekuwa Rais ambaye hakai chini katika utendaji. Sasa kama Rais anakosa muda wa kupumzika wewe wa chini utalalaje?Ó anahoji Prof. Ishengoma.
Anasema pia katika nyanja za kiusalama, Serikali ya Kikwete imefanya jitihada na imefanikiwa kupunguza nguvu za ujambazi.ÒUsalama wa raia upo ingawa sehemu za Magharibi bado kuna tatizo.Ó
Lakini je, vipi kuhusu tatizo la umeme linalowakabili Watanzania na uchumi wao? Prof. Ishengoma anasema si jambo jema kumtupia lawama Rais Kikwete pekee.
ÒTusimtafute mchawi, hili suala la umeme lina uhusiano mkubwa na mazingira. Sisi tunazalisha umeme wa maji, watu wanaharibu mazingira unategemea nini?
ÒHatuna reserves za majiÉlazima tujifunze kutunza mazingira na hili si la kuzembea kabisa ni vizuri kuvisaidia vyanzo vya maji.
ÒMimi nipo Morogoro tangu mwaka 1973 wakati huo kulikuwa na maji yanatiririka milimani na hata marehemu Mbaraka Mwinshehe aliimba. Leo hii hakuna kitu kama hicho. Tuwajibike sasa kwa pamoja.Ó
Anapozungumzia suala la Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, anasema Watanzania hawana haja kuwa waoga na muungano huo.
ÒNi kweli tuna suala la Muungano wetu na Zanzibar ambalo linasumbua kidogo, lakini huwezi kukataa Jumuiya kwa kigezo cha Zanzibar.
ÒTunatakiwa kuelewa kuwa kuna mambo ya bed room (chumba cha kulala) na sitting room (sebuleni) sasa mazungumzo ya vyumba ni tofauti kabisa.
ÒKuleta hoja ya woga hapa huu ni ujinga na hatuwezi kusema kuwa hatuendi huko. Sisi kama nchi hatuwezi kukwepa mabadiliko. You change or changes will change you. Mimi naona tusisubiri mabadiliko yatubadilishe ni heri tubadilike sasa,Ó anasema na kuongeza:
ÒDunia inakwenda na wakati kwa njia ya muungano. Sasa kama dunia inaungana sisi tunasubiri nini?
ÒSuala hapa basi liwe ku-survive na tujiulize how do we join. Je, tunakubaliana nini huko? Tunafanyaje? Lakini isiletwe hoja ya kipuuzi kwamba tukwepe kuungana. Tutakwisha.Ó
Anaongeza kuwa jambo la msingi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuangalia Tanzania inapeleka kitu gani sokoni. Anasema kwa mfano kama Wakenya wana uhaba wa mahindi ni jukumu la Watanzania kulima mahindi na kuyasambaza katika soko la Kenya.
ÒMbona leo hii tunakula apples za Afrika Kusini? Hapa sasa tuangalie nafasi yetu kisoko na si kukwepa muungano huu.Ó
Mbali na kuungwa kwake Jumuiya ya Afrika Mashariki, Prof. Ishengoma ni mtu wa karibu anayependa kuona wanawake wanapewa nafasi katika jamii.
Anasema si jambo jema kuwafungia wanawake kwenye chupa. ÒWape uhuru waonyeshe vipaji vyao na tuache dharau dhidi yao.Ó
Lakini kuna jambo jingine linalomkera sana. Nalo ni vijana kupotoka kimaadili. Anasema vijana wengi wanataka kuwa Wamarekani; hawautaki Utanzania.
ÒWako brain washed kabisa lakini wameharibiwa na sinema wanadhani kuwa hayo ndiyo maisha halisi. Vijana hawa ni kama kuku broilers, sisi tunataka kuku wa kienyeji.Ó
Katika maisha ya kawaida, Prof. Ishengoma ametumia elimu yake ya misitu kuyatengeneza mazingira ya makazi yake.
Kuna miti mbalimbali mojawapo ni cacao ambao wengi wanaamini kuwa miti hiyo haiwezi kustawi hapa nchini. Ana miti aina ya mdalasini, miembe na bwawa la samaki.
Kimsingi hakuna zao la bustani ambalo utalikosa kwa Prof. Ishengoma na anajivunia jambo hilo na kwamba amefanya hivyo kupunguza gharama za maisha.
ÒLitakuwa ni jambo la ajabu sana kama nitakwenda sokoni au mtu wa familia yangu anakwenda sokoni kutafuta nyanya, ndizi au pilipili. Nina kila kitu humu ndani,Ó anasema Prof. Ishengoma.
Profesa Ishengoma alizaliwa mkoani Kagera Aprili 4, 1952 alikopata elimu yake ya msingi kabla ya kujiunga na sekondari ya Nyakato mkoani Mwanza.
Alimaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Mazengo mkoani Dodoma mwaka 1972 na mwaka uliofuata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kampasi ya Morogoro ambayo baadaye ndiyo ilizaa SUA.
Mwaka 1986 alipata udaktari wa sayansi ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Norway na mwaka 1996 akawa profesa kamili. Msomi huyo ambaye yuko kazini kwa miaka 30, mke wake ndiye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma.

Zemkala, Machifu, Maembe na Usiku wa Umoja

na innocent munyuku

MKUSANYIKO wa muziki wa reggae, midundo ya ngoma za asili kutoka kwa kundi la Zemkala na Bagamoyo Pirits ni mambo yanayoanza kulitikiza jiji la Dar es Salaam kiasi cha wiki mbili zilizopita.

Pengine niseme kuwa mashabiki wa muziki wamezoea mkusanyiko kama huo kuwa kwenye matamasha maalumu na si mazoea ya kila wiki. Lakini sasa hilo limewezekana baada ya Umoja Entertainment kuanzisha Usiku wa Umoja unaofanyika kila Ijumaa kwenye Ukumbi wa Art Gallery Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Ni usiku wa mseto wenye kila aina raha kwa mashabiki wa muziki. Naam ndivyo ulivyo kutokana na mchanganyiko wa vipaji wasanii wa aina mbalimbali. Kuanzia wataalamu wa reggae, ngoma za asili na Madj wenye ujuzi wa kuwarusha mashabiki kwa staili nyingine za muziki kwa mtindo wa disko.

Lakini ukiachana na muziki wa Dj, cha kufurahisha ni mkusanyiko wa vichwa vyenye ujuzi wa muziki. Hawa ndio wasanii halisi waliopikwa wakapikika na wamedhihirisha hilo katika ulimwengu wa medani hiyo katika kona nyingi za dunia.

Tuanze na kundi la Zemkala. Hawa ni vijana wananane waliojikusanya kwa nia ya kuzinadi ngoma za asili. Zemkala ni neno la Kiyao likiwa na maana ya maendeleo.

Lije jua au mvua Zemkala hawana masihara kwenye kazi na ndio maana katika Usiku wa Umoja huko Art Gallery mashabiki wanapagawa kwa staili yao ya uimbaji na uchezaji wa ngoma za asili.

Kundi hilo linawajumuisha Yuster Nyakachara, Havintishi Baraza, Fadhili Mkenda, Yusuf Chambuso, Maulid Mastir, Kasembe Ungani, Shabaan Mugado na Fred Saganda.

Unapopigwa wimbo wa Tuvine (Tucheze) waweza kudhani kuwa jukwaa linasambaratika muda huo kutokana na kishindo kikuu cha ngoma za vijana hao ambao hawajavuka umri wa miaka 30.

Katika onyesho la Ijumaa iliyopita wakati mwendesha shughuli alipotangaza kuwa Zemkala walikuwa wanajiandaa kuvamia jukwaa na midundo ya asili, baadhi ya mashabiki pengine kwa ile dhana ya kubeza muziki wa utamaduni walianza minongÕono ya kutoridhika.

Lakini baada ya kundi hilo kuanza kuonyesha umahiri wao, hapakuwa na kuangalia pembeni zaidi ya kuwakodolea macho wasanii hao na kuwasindikiza kwa vifijo na nderemo. Huo ukawa ushindi kwa Zemkala dhidi ya fikra potofu zinazojali muziki wa kigeni.

Kabla ya Zemkala, kulikuwa na onyesho kutoka kwa Bagamoyo Pirits linaloongozwa na msanii kinara Vitali Maembe ambaye Jumamosi hii anamalizia stashahada yake kwenye Chuo cha Sanaa cha Kimataifa cha Bagamoyo.

Kama ilivyotarajiwa, Maembe na kundi lake wakiwa na mtindo wao wa Motokaa, waliwakumbusha mashabiki uhondo wa kibao cha Sumu ya Teja na hivyo kuwateka nyoyo mashabiki.

Ukiachana na hao, wengine waliokamilisha Usiku wa Umoja ni kundi la reggae la Machifu. Kazi ya wasanii hawa kwa hakika iliwashangaza wengi kutokana na ukweli kwamba si kundi linalofanya mazoezi ya pamoja.

Kila mmoja yu katika pilika zake na ikifika siku ya onyesho kila muhusika hukumbatia majukumu yake jukwaani na si rahisi kujua kuwa hawako pamoja katika mazoezi ya kila siku.

Wanapoimba kibao cha Julia moja kwa moja kutoka jukwaani si rahisi kujua watu hawa hawana mazoezi ya muda mrefu katika maisha yao. Hukutana saa chache kabla ya onyesho.

Ni wanamapinduzi, waliojaa fikra za kumkomboa mtu Mweusi kutoka kwenye makucha ya watu wa Magharibi. Makucha ambayo kwa miaka mingi yameendelea kuwaumiza Waafrika kwa kisingizio cha ustaarabu.

Hawa ni wakombozi wanaotumia magitaa, vinanda na sauti zao katika kuwalaani mafisadi wanaendelea kuikandamiza nafsi ya mnyonge si ndani ya Afrika tu bali duniani kote kunakohubiriwa upendo.

Lakini nini hasa kiini cha kuleta Usiku wa Umoja? Mwasisi wa usiku huo, Gotta Warioba ameliambia gazeti hili kuwa lengo ni kuwapa mashabiki mseto wa burudani.

ÒHili wazo ni la muda na nimekuwa nikiwaza kuwa kuna umuhimu wa kuwa na kitu kama hiki kwa sababu bila mkusanyiko wa aina hii hatuwezi kufika mbali.

ÒUmekuwa shahidi hapa. Wasanii wamepiga reggae, ngoma za asili na huu ni mwanzo tu nadhani katika siku zijazo tutakuwa na ladha tofauti tofauti zaidi,Ó anasema Gotta.

Lakini mbali na kuwakusanya mashabiki kwa lengo la kuonyesha uwezo wao, Gotta anasema huo ni mwanya kwa vikundi kuendelea kuwa katika joto la jukwaa kila leo.

Anasema si jambo zuri kwa msanii kusubiri mialiko ya msimu wakati upo uwezo wa kuwakutanisha kila wiki. Kwamba mbali na kubadilishana mawazo, mkusanyiko kama huo ni sawa na kisima cha ujuzi kwa wasanii.

Je, wasanii wenyewe wanasemaje kuhusu Usiku wa Umoja? Maembe anaeleza kuwa amefarijika kutokana na utaratibu huo kwa sababu mbali na kujitangaza, wanapata fursa ya kuona mwamko wa mashabiki dhidi ya kazi za sanaa.

Kauli kama hiyo haina tofauti sana na Kasembe Ungani wa Zemkala. ÒTumekuwa tukisubiri sana mambo kama hayaÉhapa unazidi kuwa mwenye hamu ya kuendelea na sanaa kwa sababu unapata changamoto za kila aina.Ó

Lakini kwa mujibu wa Ungani changamoto pia kwa watu wengine wanaojitangaza kuwa wasanii wakati hawana ubunifu wowote.

ÒSisi hapa umeona tunapiga kazi moja kwa moja hakuna anayetumia CD kuimba, watu wanapiga vyombo kwa ubunifu mkubwa. Hii ndiyo tofauti na hao wengine,Ó anaeleza.

Anasema kutokana na hilo ni vema wanaodhani kuwa wasanii wakajipanga upya kwani kuimba pasipokujua upigaji wa ala mbalimbali na elimu ya muziki kwa ujumla ni kujidanganya.

Kwa mtazamo wangu, usiku huu usiwe kama mbio za sakafuni. Wasanii pamoja na waandaaji waendelee kulitangaza jina la sanaa kwa ubora unaosubiriwa na mashabiki.

Ni wazi kuwa kama mjumuiko wa aina hiyo utaendelea kuimarishwa, wasanii watakuwa na nafasi nzuri ya kujiimarisha katika kazi zao za kila siku kwani umoja daima ni nguvu.

Umoja una umuhimu mkubwa katika maisha ya mwanadamu na hilo limewekwa kwenye maandiko ya Biblia na Quran pia. Kwamba tuwe na umoja ili kujenga uhusiano mwema daima.

munyuku@gmail.com
0754 471 920

Kirigini: Serikali ya Tanganyika itarudi

na innocent munyuku

HERMAN Kirigini si jina geni katika ulimwengu wa siasa nchini Tanzania. Ameshaliwakilisha bungeni jimbo la Musoma Vijijini kuanzia mwaka 1975 hadi 1985. Hivi karibuni mkongwe huyo wa siasa amezungumza na RAI katika mahojiano maalumu kuhusu mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kagusia Muungano na kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.

Akizungumzia juu ya mchakato wa Shirikisho la Mashariki, Kirigini anasema kimsingi watawala wa nchi zote tatu yaani Kenya, Uganda na Tanzania wamewaburuza wananchi wake.

Kwa mtazamo wake, nchi kama Tanzania inaburuzwa kuingia katika muungano huo na kwamba rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa anastahili lawama kwa kuridhia jambo hilo.

“Huyu wa kwetu niseme kwa uwazi kabisa aliburuzwa. Ndiyo! Mkapa aliburuzwa kwa sababu alikuwa dhaifu,” anasema na kuongeza kuwa Tanzania inakimbilia huko pasipo kujua udhaifu wao kiuchumi.

Anasema kuwa kwa kasi ya ukuaji wa uchumi unaofanywa na Kenya ni wazi Tanzania itamezwa katika jumuiya hiyo.

Kwamba Tanzania na Uganda si ajabu zikawa dampo la bidhaa kutoka Kenya kutokana na takwimu za mwaka uliopita juu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Mwaka jana, Kenya iliiuzia Tanzania na Uganda bidhaa mbalimbali za viwandani zenye thamani ya dola za Marekani milioni 593.351 wakati Tanzania na Uganda zikiiuzia Kenya bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 186.200.

Katika mwaka huo huo, Uganda na Tanzania ziliagiza kutoka Kenya bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 638.992 na hii kwa mtazamo wa Kirigini nchi hizi hazina uwezo sawa kiushindani.

“Uchumi wa Tanzania na Uganda unategemea zaidi kilimo cha mazao wakati ule wa Kenya ukitegemea viwanda na huduma,” anasema Kirigini na kisha kuongeza:

“Hali hii inaufanya uchumi wa Kenya kuwa imara zaidi kushinda wa Tanzania na Uganda unaotegemea hali ya hewa wakati ule Kenya ambao daima unategemea uzalishaji wa bidhaa za viwandani.”

Lakini pia Kirigini anasema kuwa nchi hizi tatu katika suala la mapato na bajeti zake kwa mwaka hayalingani. Kwamba Kenya inapata dola bilioni 3.715 na matumizi yao ni dola 3.88.

Tanzania inapata dola za Marekani bilioni 2.235 huku matumizi yake yakiwa dola 2.669. Uganda inapata dola bilioni 1.845 na inatumia dola bilioni 1.904 kwa mwaka.

“Ndiyo maana nasema wananchi wanaburuzwa na viongozi wa kisiasa katika jambo hili,” anasema.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa hili suala la watu kutangaza kutaka maoni juu ya wananchi kuhusu shirikisho ni hadaa kwani maamuzi yalishafanywa.

“Leo hii unawauliza wananchi inasaidia nini? Hii ni hadaa, wangepewa nafasi ya kwanza kutoa maoni. Hivi kweli hatukumbuki tulivyoumia baada ya Jumuiya ya awali iliyovunjika mwaka 1977? Nani walifaidika zaidi kama sio Wakenya?”

Anasema wakati jumuiya inavunjika njia kuu za uchumi zilikuwa zikishikiliwa Kenya na wao wakaziendeleza kwa maslahi yao.

“Tuliumwa na nyoka na je, leo tuna uhakika gani kama muungano huu hautavunjika?” anahoji Kirigini.

Akizungumzia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kirigini anaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ameachwa peke yake.

“Kikwete analia peke yake katika kutatua mgogoro wa kisiasa Visiwani na kasoro za Muungano. Hawa viongozi wa CCM hawampi ushirikiano kukemea maovu ya Zanzibar.

“Kasimama bungeni (Kikwete) na kusema kuwa kuna mpasuko wa kisiasa Zanzibar lakini mbona hawamsaidii kuyakemea?

“Zanzibar kuna tatizo kubwa sana, Karume ni sawa na Salmin Amour wanalewa madaraka.”

Anasema kutokana na kasoro hizo ipo siku hoja ya Serikali ya Tanganyika itaibuka upya.

“Mimi nasema Serikali ya Tanganyika lazima itarudi na kosa alilofanya Nyerere ni kutokubali kubaki na Tanganyika, amefariki dunia akilijua hilo na hakuweza kurudi nyuma,” anasema Kirigini.

“Lakini mbali na jambo hilo, jambo jingine ni kwamba wengi waliomfuata Nyerere walikuwa wanafiki, walimwogopa badala ya kumshauri.

“Mimi sikutaka kuwa katika mkumbo huo na ndio maana wakati fulani bungeni nilichachamaa kwa kuwatetea wakulima wa pamba.

“Hili si Bunge, nakumbuka katika utetezi wangu kwa wakulima, Mwalimu alitaka kunikamata, alidai mimi na wenzangu tunapinga chama ndani ya Bunge.”

Anasema alichofunza katika miaka yake kama mwanasiasa ni kwamba CCM haitaki kuukubali upinzani na kutokana na misimamo yake, wana-CCM wengi wamekuwa wakimtenga kwa kumwona msaliti.

“Mwaka 1987 niliomba ujumbe wa NEC nikapewa alama ya E na kwamba mimi ni msaliti wa kisiasa, nikaandika barua Halmashauri Kuu lakini hadi hii leo sijajibiwa.

“Nikaonekana mbaya kwa watu wa mkoa wangu lakini upinzani ule leo hii ndio huo ambao umekubalika. Kuna chama kama CUF ni vema kikaendelea kuwepo ili pawe na criticism.”

Anaeleza kuwa mawazo makongwe hasa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wasiokubali mabadiliko yamesababisha CCM wakati mwingine kukosa mwamko.

“Lakini bado nakubali kwamba hawa walioko CCM baadhi yao wakitoka na kuunda chama kingine chama hicho kitakuwa bora kwani wapinzani wa kweli wangali humo.”

Kuhusu mwaka mmoja wa Serikali ya Kikwete, Kirigini anaeleza kuwa mtawala huyo anakubalika na wengi lakini kasi yake wengi hawaiwezi.

“Kikwete ana kasi ya ajabu na mtu mzuri lakini watu wake (viongozi) hawaendi naye. Wameachwa nyuma na kama mpiganaji, anatakiwa arudi nyuma aangalie majeshi yake mfano ni hizi Serikali za Mitaa zimeoza.”

Hata hivyo, anapingana na utaratibu wa Serikali kuwachangisha wananchi kwa ajili ya sherehe za Uhuru. Anasema kimsingi ni heri jambo hilo likawa katika bajeti.

“Waliochanga wengi ni wafanyabiashara na kwa kawaida wafanyabiashara hawana nia nzuri, wanakuwa na lao jambo.”

Kirigini ambaye kitaaluma ni Bwanashamba alizaliwa Desemba 22, 1955 ameoa na ana watoto wanane mmoja kati ya hao ni Rosemary Kirigini ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).

Kirigini amewahi kuwa Waziri wa Mifugo kati ya mwaka 1980-83 na kati ya mwaka 1983-85 akawa Waziri wa Nchi anayeshughulikia mifugo.

Amewahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga na Arusha kati ya mwaka 1993-96. Ana shahada ya kilimo aliyoipata Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 1970.

Raila kapiga zumari Kenya, tulicheze Tanzania

na innocent munyuku

WANASEMA uzee ni dalili ya hekima lakini pamoja na ukweli huo uzee hauhalalishi kuziba vipaji au mianya ya wengine kuonyesha uwezo wao katika masuala mbalimbali yahusuyo jamii. Basi tuseme pia katika hili uzee waweza kutumika kama mwongozo au mifano sahihi kwa ustawi wa jamii.

Katika hilo ndio maana hadi hii leo kwa baadhi ya kaya huwatumia wazee katika kufanya suluhisho kwenye eneo husika hasa kama kutatokea kutokuelewana baina yao. Pengine kutokana na hilo inawezekana wengine wakadiriki kusema kuwa ukubwa ni jalala.

Lakini katika nyanja za siasa hasa barani Afrika hali ni tofauti. Wazee wameonyesha njia mbaya kwa kung’ang’ania madaraka na huu kwa mtazamo wa kawaida kabisa ni ishara na mwongozo usiofaa kwa vijana wanaochipukia katika siasa na hata waliosimama kabisa.

Nimeamua kuandika haya kwa kusimamia hoja ya Mbunge wa Jimbo la Lang’ata nchini Kenya, Raila Odinga aliyependekeza hivi karibuni kuwa ni vema wanasiasa wa nchini mwake ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu waachie ngazi na kupisha damu changa.

Odinga alisema kuwa anashangaa kuwaona wanasiasa wa jinsi hiyo ambao hadi hii leo wangali wakishika utawala tangu enzi ya marehemu baba yake Jaramongi Oginga Odinga.

Ingawa Odinga alikuwa akiyasema hayo kukipigia debe chama chake cha Orange for Democratic Movement-Kenya (ODM-K), maneno yake yalitosha kuwa changamoto kwa ajili ya kujenga vyama vyenye damu mpya na mawazo mapya katika siasa.

Nchini humo kwa mfano, Makamu wa Rais Moody Awori ana umri wa miaka 79, huku kukiwa na mawaziri wengine wenye umri mkubwa kama yeye akiwemo Njenga Karume (80), Simone Nyachae (75) na John Michuki (74).

Kimsingi hoja ya Raila si ya kuachwa ipite hivi hivi pasipo kuungwa mkono na katika hili ndio maana nasema kuwa mwanasiasa huyo machachari amelenga sehemu husika kutokana na ukweli kwamba sehemu mbalimbali barani Afrika lina tatizo kama hilo.

Tanzania kama ilivyo Kenya pia ina wanasiasa ambao leo hii wana rekodi ya kubakia katika ulingo huo huku wakiziba ya damu changa zisiweze kuonyesha upeo wao katika nyanya mbalimbali. Hao wamejaa tele na ni kama wamepigiliwa misumari.

Ndani ya Tanzania wapo wanasiasa ambao tangu wengine hatujazaliwa wapo katika ulingo huo wakiendesha maisha yao kwa mgongo wa siasa na hadi hii wangali madarakani kama vile hakuna Mtanzania kijana mwenye uwezo wa kuyatenda hayo ayatendayo huyo aliyeko madarakani.

Naungana na Raila kusema kuwa hii ni dalili mbaya kwa mustakabali wa taifa letu kwani ukweli ni kwamba wanasiasa wa aina hii hawana jipya katika mioyo yao. Hawana jipya la kutueleza, wamebaki na mbinu za kale ambazo kwa nyakati hizi hatuwezi kukubaliana nazo.

Kwamba hawana fikra pevu tena, vichwa vyao pamoja na kwamba wanaweza kuwa na hekima, hawana jema la kuwafundisha wengine. Ni heri kwao wakakubali mabadiliko kuliko kung’ang’ania siasa. Huu uwe wakati wa kuwafundisha wengine. Na kufundisha kuzuri ni kwa kumpisha mwanafunzi kitini na kumwelekeza namna ya kuliongoza jahazi.

Kama wanasiasa wa jinsi hii wameshindwa kuleta maendeleo au kuishauri Serikali husika kwa kipindi cha miaka 20 au 30 leo hii watakuwa na miujiza gani katika kulisukuma gurudumu mbele gurudumu la maendeleo na tija halisi kwa Watanzania?

Hawa wazee wa siasa wana jipya gani leo hii? Watasimama waseme kitu ambacho kwa wakati huu watu watakubali kuwa wanachokinena ndicho sahihi? Lakini hakuna shaka kwamba salamu wamezipata wakati ule wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Baadhi yao nasikia walizomewa na wakalazimika kushuka jukwaani wakiwa wamevaa sura za aibu.

Hivi kwani ni lazima wote wawe wanasiasa? Kwanini wengine wasibaki pembeni na kuangalia vichwa vingine vikiongoza jahazi? Bila shaka zumari la Raila lafaa lisikizwe kwa makini na lichezwe hapa kwenye ardhi yetu ya Tanzania. Tusipuuze kwani alichokisema nchini Kenya ndicho kilichopo hapa kwetu.

Sileti siasa za kibaguzi lakini kwa mtazamo, ufike wakati wazee wakubali mabadiliko si kwa kuwapiga watoto wao (wa damu) bali pia kuwapa nafasi wengine wajaribu kujiwekea rekodi zao. Ninachotarajia kwa muda huu ni hawa wazee wajenge vitalu bora kwa kuwapika vijana kisiasa badala ya kuwawekea vizingiti ambavyo kimsingi vinaliangamiza taifa.

Kwamba wakati huu uwe mwafaka kwa Watanzania kujifunza kutokana na changamoto ya kina Raila na kundi lake. Kwani hawa vijana wasipojifunza leo watapata wapi nafasi hiyo? Wasipojaribu leo watajaribu lini?

Tusione aibu kuwapisha vijana waonyeshe walichonacho kwenye vichwa vyao na kama watateleza huo utakuwa muda mwafaka kuwarekebisha na kuwaelekeza wapite wapi na watufikishe wapi. Kuwabana ni kuwanyima haki yao na huu si utaratibu mzuri wa kukuza maendeleo. Tuwape nafasi hii leo.

Niseme pia kuwa hatujachelewa kufikia kuwapa vijana nafasi. Ni suala la maandalizi ambayo yakianza sasa bila shaka katika Uchaguzi Mkuu ujao wazee watakubali kukaa pembeni na kuwapisha vijana waendelee kukimbiza kijiti cha maendeleo.

Hakika tusione aibu kabisa kuanza kulicheza zumari la Raila. Huo ndio uungwana, kubalini mabadiliko mapema ili heshima yenu isipotee.

munyuku@gmail.com

Sunday, November 26, 2006

Tuchangie harusi hadi lini?

na innocent munyuku

KIASI cha miaka miwili nyuma, rafiki yangu wa karibu alipata kuniambia namna alivyojijengea ukuta mgumu dhidi ya ndugu, jamaa na marafiki baada ya kuweka wazi msimamo wake juu ya kutochangia harusi.

Katika simulizi zake, jamaa huyo akanieleza kuwa ilifika mahala akashindwa kuchangia pesa kwa ajili ya harusi kwa vile aliangalia hesabu ya bajeti yake kwa mwezi, akakuta anatumia kiasi kikubwa cha pesa katika kuchangia harusi badala ya mambo mengine ambayo anaamini ni ya msingi zaidi.

Akatoa mfano kwamba kama kila mwezi watu sita wanaoa au kuolewa na kila mmoja atamchangia Sh 20,000 ina maana kila mwezi atenge Sh 120,000. Hivyo basi kwa mwaka mzima itamgharimu Sh 1,440,000. Hiyo ilikuwa miaka miwili iliyopita na kuna uwezekano mkubwa gharama kwa ajili ya shughuli hizo zimepanda.

Nimelazimika kuandika makala hii kutokana na kuguswa na hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida na ukweli kwamba, kila siku michango ya harusi imeendelea kushamiri miongoni mwetu.

Kwamba kwa vile gharama ya maisha imepanda kwa kiwango kikubwa ni heri tukaangalia maeneo muhimu ya kuchangia ili kuleta tija kwa kila Mtanzania. Nasema hivyo kwa sababu dhamira yangu inanituma kuamini kuwa, michango mikubwa katika harusi haina neema kwa wahusika. Kama kuna wanaonufaika katika michango hiyo ni wachache na kwa muda mfupi.

Imebainika kuwa, michango mingi hasa ya pesa huishia kwa waliochangia na si kwa maharusi. Kwamba fedha zinazokusanywa hatimaye huishia kwenye matumbo ya waliochanga kwa kunywa na kula siku ya harusi na baadaye kile kinachoitwa kuvunja kamati.

Binafsi ningeunga mkono kuendelea kwa michango hiyo kama pesa zingewanufaisha moja kwa moja maharusi. Kwa mfano zimepatikana shilingi milioni nne basi wapewe maharusi kwa ajili ya kuendelea na maisha yao.

Ya nini basi tuchangishane mamilioni ya pesa halafu tuzitumbue pesa hizo kwa kunywa bia na kula pilau? Kuna maana gani basi kuwaona maharusi baada ya siku chache wanalia njaa kwa sababu pesa zimeshatumika kukamilisha sherehe ya wao kuungana katika ndoa? Ni heri tubadilike sasa kwani huko tuendako siko.

Nitatetea hoja yangu hii kwa msingi mkuu mmoja nao ni kuwa, naamini wanaojiandaa kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria wamefikisha umri wa kufanya hivyo na wanapojiandaa katika muungano huo wa hiari wawili hao wameshaweka maandalizi ya maisha yao mapya.

Kwa maana hiyo, katika mazingira kama hayo ni jambo lililo wazi kuwa wanaooana lazima watakuwa kwenye nafasi ya kukabiliana na majukumu ya ndoa ikiwa ni pamoja na maisha ya kila siku. Wanachotakiwa ni kujiandaa kama afanyanyo mwanafunzi darasani kukabiliana na mitihani yake.

Si mara moja au mbili, kumekuwa na matukio ya kuchefua roho baada ya kumalizika kwa harusi. Utasikia bwana na bibi harusi wanakabiliwa na madeni yaliyotakana na ‘kuzidi kwa bajeti’ ya harusi yao. Wanabaki kukuna vichwa wasijue watalizipaje pesa hizo. Huu si uungwana!

Kwa hakika si uungwana na ndio maana napiga zumari hili lenye sauti ya kupinga kuchangishana pesa kwa ajili ya harusi na baadaye kuzitumia pesa hizo kwa ajili ya kushibisha matumbo na kuwaacha wanandoa ambao ni wahusika wakuu wa shughuli hiyo wakienda nyumbani mikono mitupu.

Kama kweli tuna mapenzi ya dhati na maharusi kwa nini basi pesa zinazochanganywa wasipewe ili wajue nini cha kufanya mara baada ya kutoka kwa kasisi au sheikh? Huu ni muda wa kubadilika, matarumbeta na kukodi kumbi za kifahari tuwaachie wengine ambao wana uwezo wa kutenda pasipo kutembeza bakuli.

Badala yake tuchangie katika masuala mengine ambayo naamini kuwa ni muhimu kuliko hili la kuchangishana ili watu wapate kushiba kwenye harusi. Tulipe mgongo suala la harusi na tuangalie maeneo mengine kama elimu au afya.

Kuna mifano hai kwamba, wapo watu walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu tu hawana pesa za kuwawezesha kusonga mbele. Hao wamejaa kwenye ardhi ya Tanzania. Wamefumbiwa macho kwa sababu dhamira za walio wengi ni kutoa pesa ambayo baada ya mwezi mmoja ataitumia kwa kunywa bia na kutafuna vipapatio vya kuku.

Jaribu leo kuitisha kikao kwamba unataka kujiendeleza shule na unahitaji kuchangiwa pesa kwa ajili ya kukidhi gharama za masomo. Hata marafiki zako wa karibu wanaweza kukupiga chenga. Naam watapiga chenga kwa sababu huo utamaduni ni mpya katika mioyo yao. Wamezoea kuchanga ili siku chache baadaye wazirejeshe pesa hizo kwa faida yao. Hawaangalii matokeo mema yanayolengwa kuja kwa miaka walau minne ijayo.

Naamini kabisa kuwa pesa zinazotumika katika kufanikisha harusi zingewasaidia wahitaji wengine kama wagonjwa waliolazwa hospitalini. Inawezekana wakajitokeza wengine wakadai kuwa hilo ni jukumu la Serikali. Huko ni kupotoka, kwani kama tuna ubavu wa kufanya harusi za kifahari kwa kuchangishana pesa kwanini tushindwe kuwasaidia watu wengine katika masuala muhimu?

Leo hii nikiamua kwenda kanisani kufunga ndoa na kisha kuingia kwenye banda langu la uani na mke wangu bado nitakuwa na amani kwamba jambo la msingi limeshafanyika nalo ni uhalali wa ndoa hiyo mbele ya kasisi na baraka kutoka kwa mashuhuda wanaotambulika kwa mujibu wa sheria. Sitakuwa na kinyongo bali furaha tele moyoni.

Watanzania tumekuwa wepesi wa kuiga mengi kutoka Ulaya na Marekani kwanini basi utaratibu wa ndoa za ‘kimya kimya’ nao tusiige kutoka kwao? Kwamba huko ughaibuni mtu anajikuna anapofikia na kufanikisha harusi yake na wala hana haja ya kulia shida kwa wengine. La maana ni cheti cha ndoa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

epuka utumwa wa akili

Thursday, November 16, 2006

Zemkala: Vichwa sita vyenye upeo wa juu
· Wasambaza ngoma za Tanzania kimataifa

Na Innocent Munyuku

UZOEFU unaonyesha kuwa watu wengi waliotimiza ndoto zao katika maisha hawakuwa na shaka na wanachowazia. Walijipanga na kuhakikisha kuwa mipangilio yao ya maisha inakuwa kama walivyokusudia. Lije jua au mvua.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa wasanii wa ngoma na nyimbo za asili ya Tanzania wanaojulikana kama Zemkala. Ni kundi linaloundwa na wasanii sita ambao bado umri wao haujavuka miaka 30. Wangali na damu mbichi katika kueneza mila na utamaduni wa Mtanzania katika nchi mbalimbali duniani.

Wanaounda kundi hilo ni Yuster Nyakachara, Havintishi Baraza, Fadhili Mkenda, Yusuf Chambuso, Maulid Mastir na Kasembe Ungani.

Kwa mujibu wa kiongozi wa kundi hilo, Yusta Nyakachara, walianza kupata uhai mwaka 2002, waanzilishi wakiwa Ungani na Mkenda ambao walijieungua kutoka katika kundi lililowahi kuvuma wakati la Sisi Tambala. Wasanii wengine walijumuika na Zemkala wakitokea Splendid Theatre.

Katika miaka minne ya uhai wa kundi hilo, Zemkala imefanya mambo mengi ndani na nje ya nchi kwa kulitangaza taifa katika maonyesho ya sanaa kila lilipopata nafasi ya kufanya hivyo.

Cha kufurahisha kuhusu wasanii hawa ni kwamba si rahisi kujua kama wamepeana majukumu tofauti jukwaani. Hawana mzaha wawapo katika pilikapilika za kuleta burudani huku kila mmoja akijaribu ‘kuivaa’ kazi ya msanii mwingine.

Chambuso ni hodari katika kupiga ngoma nane, lakini usishangae kumwona akiziacha ngoma hizo na kujiunga na wachezaji ambao ni Yusta na Havintishi ambao ni mahiri katika kulishambilia jukwaa.

Si Chambuso tu mwenye hulka hiyo, Mastir ambaye ni kiboko ya njia katika kupiga marimba, hasiti kuacha marimba hayo na kuwavaa mashabiki akiwaonyesha uwezo wake mwingine wa kucheza na kuruka sarakasi na baadaye atamweka pembeni Chambuso naye kuanza kupiga ngoma tena kwa ustadi mkubwa kabisa. Wakati huo filimbi yake inakwenda pamoja na mirindimo ya drums kutoka kwa Mkenda.

Lakini uhondo huo unakuwa haujakamilika pasipo kumhusisha Ungani. Huyu ni kinara katika kupiga ngoma ndogo maarufu kama jembe. Mara chache utamwona akicheza lakini uso wake wa tabasamu na umakini utakufanya mara kwa mara kuangalia namna anavyokwenda vyema na wapigaji wa vyombo vingine.

Tangu kuundwa kwa kundi hilo, wameshazuru Sweden, Msumbiji, Kenya na Zanzibar katika kufanya maonyesho mbalimbali kupitia matamasha ya sanaa. Huko kote wameacha sifa njema na kujizolea mashabiki lukuki.

Unapowauliza katika maonyesho hayo ni lipi ambalo wanalikumbuka zaidi hawasiti kulitaja onyesho la mjini Kisumu kiasi cha miaka miwili iliyopita. Kwa nini wanalikumbuka? Swali kama hilo linawafanya wote waangue kicheko kinachofuatiwa na maelezo kutoka kwa Yusta.

“Kule katika siku ya kwanza ya maonyesho yetu tulipata wakati mgumu sana. Unabadilisha nguo hapo ili uvae za kuingilia jukwaani unasikia mtu pembeni yako akisema ‘cheki hiyo bonge ya raba lazima tutoke nayo.

“Sasa katika mazingira hayo unapanda jukwaani pasipo umakini, kwani unawaza kuibiwa viatu au vifaa vingine,” anasema Yusta.

Lakini baada ya kulalamika kwa waandaaji wa shughuli hiyo mambo yakabadilika siku iliyofuata. “Hata hivyo, bado ikawa adhabu kwetu…ni sawa tulipewa ulinzi wa kutosha lakini shughuli ilikuwa pevu,” anakumbuka Mastir.

Kwamba kwa vile onyesho lao lililotangulia walivipiku vikundi vingine kutoka nchi nyingine, walijikuta wakiwa na mashabiki wengi ambao kila walipopanda jukwaani walilazimisha waendelee kutoa burudani pasipo kupumzika.

“Kwa hakika ilikuwa hali ngumu na kama tusingekuwa na mazeozi ya kutosha hali ingekuwa mbaya sana, unacheza jukwaani kwa dakika 60 lengo likiwa kumaliza kiu ya watazamaji wako,” anasema Yusta.

Mbali na ushujaa wao jukwaani, Zemkala wamepikwa katika msimamo wa kulinda na kujivunia utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika kwa ujumla. Maneno yao yamejawa na hamasa kama ya Dk. J Aggrey ambaye anasifika sehemu nyingi duniani kwa kujivunia ngozi yake nyeusi.

Dk. Aggrey alipata kukaririwa akisema kuwa kama angelikwenda mbinguni na Mungu angelimwuliza kama anataka kurejea duniani kama mtu mweupe angeligoma. Na kwamba kama angeulizwa kwa nini hataki kurudi kama mtu mweupe, angesema bado ana kibarua cha kufanya kama mtu mweusi na anajivunia rangi hiyo na kwamba kama kuna asiyejivunia rangi yake basi huyo hastahili kuwa na pumzi ya uzima.

Unaweza kuwataja Zemkala kuwa ni wasanii wasio na aibu kutangaza ngoma za asili ya Tanzania. Wamefanikiwa kuchanganya ngoma za makabila tofauti katika maonyesho yao kote walikopata nafasi ya kufanya hivyo.

Lengo ni kwamba ifike siku Tanzania ijulikane kupitia ngoma zake kama walivyofanikiwa Wakongo au mataifa ya Afrika Magharibi.

Wanashangaa kuona hadi hii leo baadhi ya Watanzania hasa vijana wanakataa kucheza ngoma za asili na badala yake kukimbilia disko na kuiga utamaduni wa Kimagharibi.

“Huu ni msimamo wetu kwamba lazima tuitangaze Tanzania kwa kutumia ngoma na nyimbo zetu,” anasema Yusta. “Lazima nia iwepo na wengine naamini watafuata nyayo zetu katika kujivunia mambo yetu ya asili.”

Katika jitihada zao hizo za kuing’arisha Tanzania kimataifa, wameshaanza kupenya kibiashara katika bara la Ulaya na Marekani Kaskazini.

Meneja wa Zemkala, Jotham ‘Gota’ Warioba, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa kundi hilo linasonga mbele kwa hali na mali.

Amelidokeza gazeti hili kuwa ameshaanza mazungumzo na kampuni moja ya inayojishughulisha na usambazaji wa muziki nchini Ujerumani ili kuingia nayo mkataba wa kibiashara.

Kampuni hiyo ina matawi sehemu mbalimbali barani Ulaya na kusambaa hadi Marekani Kaskazini. Hata hivyo, hakuwa tayari kuitaja kwa vile kuna mambo ya msingi wanayotakiwa kuwekana sawa kabla ya kuutangazia umma.

“Wameonyesha nia ya dhati kujumuika nasi na sisiti kusema kuwa hii ni njia mojawapo kuelekea katika mafanikio ya Zemkala,” alisema Gota.

Pamoja na hayo, Gota aliongeza kuwa anaweka mkakati wa kulifanya kundi lake hilo liwe na maonyesho ya ndani ya nchi badala ya kuwaburudisha watu wa nje pekee.

“Tanzania hakuna utamaduni wa kupenda kuangalia ngoma za asili, wamezoea dansi au disko lakini sisi tunadhani upo umuhimu wa kuwa na show (onyesho) walau mara moja kila wiki hapa kwetu ili watu waone uzuri wake…wasikimbilie kwingine.”

Zemkala hujikita katika mazoezi kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kuanzia asubuhi hadi mchana katika Ukumbi wa Utamaduni wa Russia uliopo Sea View jijini Dar es Salaam.

epuka utumwa wa akili

Saturday, November 11, 2006

Hii ndiyo moja ya hotuba mbaya za P. W. Botha

-Akiri kuwaua Weusi kwa sumu
-Atamka: Mweusi ni malighafi ya Mweupe


HII ni hotuba ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, marehemu P. W. Botha alipolihutubia Baraza lake la Mawaziri wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo. Katika hotuba hiyo iliyochapishwa katika gazeti la Sunday Times la nchini humo toleo la Agosti 18, 1985, Botha anajigamba eti ardhi hiyo ni mali yao na hawapaswi kuingiliwa. Ikumbukwe kuwa katika utawala huo, mtu Mweusi aliteswa na kunyimwa haki zake za msingi na alifanywa kuwa kiumbe kisichostahili kuishi kwa raha katika ardhi hiyo.

Pretoria imetengenezwa na watu Weupe kwa ajili ya watu Weupe na hatuna haja ya kuuthibitisha umma au mtu Mweusi kuwa sisi ni watu bora, tumekuwa tukiwaambia watu Weusi jambo hili kwa njia elfu.

Afrika Kusini ya leo haikutengenezwa katika mawazo ya kawaida, tumeitengeneza kwa kutumia akili nyingi, jasho na damu. Mnaposema kuwa tunawabagua Weusi sielewi. Hivi ni Afrikaners ndio waliojaribu kusitisha kizazi cha Aborigines wa Australia? Je, ni Afrikaners waliotenga na kuwanyanyasa watu Weusi Marekani Kaskazini kwa kuwaita niggaz?

Je, ni Afrikaners ndio waliowatenga na kuwanyanyasa watu Weusi huko England kwa kuwatungia sheria ya kuwakandamiza? Canada, Ufaransa, Russia na Japan nao wana njia zao za kibaguzi. Hivi kwa nini hasa kuna kelele nyingi dhidi yetu? Huu ni uendawazimu! Kwanini wanatukaba koo kiasi hiki? Hawatutendei haki hata kidogo.

Nataka kuwaeleza kuwa hakuna kibaya tunachokitenda hapa ambacho hao wanaojiita wako katika dunia ya ustaarabu wameacha kukifanya. Sisi ni watu wema tusio na hatia na ambao tumeweka wazi mfumo wa maisha ya tunayotaka tuishi kama watu Weupe.

Sisi sio wanafiki kama Wazungu wenzetu wafanyavyo kwamba wanawapenda watu weusi. Ukweli kuwa Weusi wanaofanana na binadamu na kutenda mambo kama binadamu hayawahalalishi wao kuwa watu wenye akili timamu au binadamu aliyetimia. Kanunguyeye si nungunungu na mijusi hawawezi kuwa mamba eti kwa sababu tu wanafanana.

Kama Mungu alitaka tufanane na Weusi angetufanya sote tuwe na rangi moja na fikra sawa. Lakini alituumba tofauti; Weupe, Weusi, Wanjano, watawala na watawaliwa. Katika upeo sisi ni bora kuliko Weusi na hilo halina ubishi kwani limejihidhirisha kwa miaka mingi iliyopita.

Naamini kuwa Afrikaner ni mtu safi, mwenye hofu na Mungu. Ni mtu ambaye ameonyesha kwa vitendo njia sahihi ya utu. Hata hivyo, inafurahisha kuona kuwa Ulaya, America, Canada, Australia na wengine wengi wako nyuma yetu achilia mbali maneno yao. Kuhusu uhusiano wa kidiplomasia, sote tunafahamu lugha inavyotakiwa kutumika. Na kwa ushahidi ulio wazi hivi kuna mtu hapa asiyejua kuwa nchi nyingi za Ulaya zinatamani kuja kuwekeza Afrika Kusini?

Nani anayenunua dhahabu yetu, nani anayenunua almasi yetu? Nani anafanya biashara nasi? Nani anatusaidia katika kuendesha silaha za nuklia? Ukweli ni kwamba sisi ni watu wao na wao ni watu wetu. Hii ni siri kubwa. Nguvu ya uchumi wetu inajengwa kwa kiasi kikubwa na America, Britain na Ujerumani. Ni jambo kubwa sana hili na kwa maana hiyo, Mweusi ni malighafi kwa Mweupe.

Hivyo basi, kaka na dada zangu hebu tuungane kumpiga vita huyu shetani Mweusi. Napiga mbiu kwa kwa Afrikaners wote kujitokeza kwa hali na mali kupigana vita hii. Kwa hakika Mungu hawezi kuwatupa watu wake ambao ni sisi. Hadi sasa imeonekana kwa vitendo kuwa Weusi hawawezi kujitawala. Wape bunduki kama hawataanza kuuana.

Hawana lolote jema isipokuwa mashujaa wa kupiga kelele, kucheza ngoma, kuoa wanawake wengi na kupenda sana ngono. Hebu sasa tukubali kuwa mtu Mweusi ni alama ya umasikini, udumavu wa akili, uvivu na aliyekosa ushindani. Hivi hapo je, si kweli kwamba mtu Mweupe aliumbwa ili kumtawala mtu Mweusi? Hivi utajisikiaje unaamka asubuhi unakuta Kaff*ir amekalia kiti cha utawala? Hivi unajua kitakachotokea kwa wanawake wetu? Hivi kuna mtu anawaza kwamba Mweusi ataitawala nchi hii.

Kwa hiyo tuna sababu nzuri ya kuwapeleka akina Mandela jela waozee huko na katika hili nadhani upo umuhimu wa kupewa pongezi kwani tungekuwa na uwezo wa kuwaangamiza lakini sasa wanaishi. Napenda kuwatangazia mikakati mipya ya kuwaangamiza hawa Weusi. Tutumie sumu kuwamaliza.

Kamwe tusiruhusu idadi ya watu hawa iendelee kukua vinginevyo tutakwisha. Tayari nimeshawaleta wanasayansi ambao wamekuja na sehemu kubwa ya mzigo wa sumu na ninawasaka watafiti wengine zaidi waangalie sehemu murua za kuitumia sumu hiyo kwa lengo la kuwaangamiza Weusi.

Sehemu nzuri za kuwaangamiza kwa sumu ni hospitali na pia katika usambazaji wa chakula inaweza kutumika. Tumetengeneza sumu inayoua taratibu na kupunguza uwezo wa uzazi. Lakini hofu yetu ni kwamba itakuwaje kama sumu hiyo itaangukia kwenye mikono yao.

Hata hivyo, tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa sumu hiyo inabaki katika himaya yetu. Pili, watu Weusi wanapenda sana pesa kwa hiyo tunaweza kuwatenga kwa njia hiyo. Wataalamu wetu wanalifanyia kazi suala hilo ili mtu Mweusi amchukie Mweusi mwenzake. Hawana upeo wa kufikiri na huyo ndiye kiumbe dhaifu kisicho na akili ya kuona mbali.

Kuna umuhimu mkubwa wa kupanga mambo hayo yaendelee kwa muda mrefu ili wasibaini kinachoendelea. Kwa kawaida mtu mweusi hapangi mikakati inayozidi kipindi cha mwaka mmoja. Na hapa napenda niwaombe kina mama wote wa ki Afrikaner wazae kwa fujo kuongeza idadi.

Litakuwa jambo la maana pia kama kutatengwa vituo maalumu ambako vijana wa kike na kiume watakaa na Serikali kuwawezesha ili wazae kwa idadi kubwa iwezekanavyo ili kuongeza idadi yetu. Wakati hilo likiendelea, lazima tuwabane watu Weusi waachane na wake zao.

Ninayo kamati inayoratibu na kuangalia njia nzuri ya kuwafanya watu hawa wachukiane na wauane wenyewe kwa wenyewe. Adhabu kwa Mweusi aliyemuua Mweusi iwe ndogo ili kuwapa hamasa ya kuendelea na mauaji.

Wanasayansi wangu wameshauri pia kuna ulazima wa kuwawekea sumu kwenye pombe, sumu ambayo itakuwa inawaua taratibu na kumaliza uwezo wa kuzaa pia. Njia kama hii na nyingine zifananazo na hii itawarahisha kuwapunguza idadi.

Rekodi zinaonyesha pia kuwa mtu Mweusi anapenda sana mwanamke Mweupe. Hii ni nafasi nzuri kwetu. Wanawake wetu warembo wanaotumika katika mbinu za kuwaangamiza wapinzani wetu watatumika kuwaua hao wanaopinga ubaguzi wa rangi.

Hili jeshi letu la mwituni la mapenzi huku tukiwa na jeshi kama hilo kwa upande wa wanaume ambao watawafuata wanawake Weusi. Pia Serikali imeagiza malaya kutoka Marekani na Ulaya kwa ajili ya kukidhi haja hiyo.

Ombi langu la mwisho ni kwamba wajawazito wanapozaa hospitalini, watoto lazima wauae pindi tu wanapotoka tumboni. Hatuwalipi wale wauguzi kwa ajili ya kutuletea watoto Weusi katika hii dunia bali kuwaangamiza.

Serikali yangu imetenga fungu maalumu la pesa kwa ajili ya kujenga hospitali na kliniki kwa ajili ya kufanikisha mpango huo. Pesa inafanya lolote na kwa vile tunazo tuzitumie ipasavyo.

Kwa muda huu ndugu zangu Weupe, msiyaweke moyoni yanayosemwa dhidi yenu na wala msione aibu kuitwa wabaguzi na wala sijali kuitwa mhandisi na Mfalme wa Ubaguzi. Siwezi kugeuka nyani eti kwa sababu mtu kaniita nyani. Nitabaki kuwa nyota inayong’aa…mtukufu Botha.

Leo naondoa mawingu; kesho nitajaribu milima!

"Maisha yetu huanza kukoma siku ambayo tunaanza kuwa kimya juu ya mambo muhimu." Dk. Martin Luther King Jr.

"Ni vema kufa kwa ajili ya imani itayoishi kuliko kuishi kwa jambo litakalokufa.” Steven Bantu Biko.

Twawapima wakuu wetu kwa mizani ya pesa?

na innocent munyuku

MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania Albert Motika maarufu kama Mr. Ebbo alipata kufyatua kibao ambacho wengi walikifurahia kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni porojo zilizojaa kwenye wimbo huo uliopachikwa jina la Mnisamehe.

Katika wimbo huo, Mr. Ebbo anaeleza baadhi ya mambo ambayo kwa akili ya kawaida hayatekelezeki na kama yatatekelezwa basi itakuwa balaa. Kama pale anaposema angefurahi kuona magazeti yote yameandikwa kwa lugha ya Kimasai au mnada wa ng’ombe wa Pugu usogezwe hadi Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam.

Lakini msanii huyo anaendelea kuimba kwamba hata gari moshi zisiwe na honi kwenye safari zake na anaomba apande gari lisilo na breki. Kila anachosema mwisho wake humalizia kwa kutaka asamehewe kwa kauli yake hiyo. Bila shaka ujumbe ulishafika!

Nami kabla sijajikita katika msingi wa makala yangu hii leo naomba nisamehewe kwa hoja yangu kwamba tuzo kwa marais wa nchi iliyoandaliwa na tajiri Mohamed Ibrahim kwa mtazamo wangu sioni kama imelenga kufichua ama kuutokomeza ufisadi katika Afrika.

Kwa zaidi ya wiki moja sasa, vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikiandika kwa kina taarifa hiyo ya tajiri huyo anayependa kuitwa Mo Ibrahim ambaye asili yake ni nchini Sudan ingawa mwaka 1975 alipewa uraia wa Uingereza.

Tajiri huyo bila shaka kwa nia njema kama alivyoona katika dhamira yake ametangaza kuanzishwa kwa tuzo maalumu ya marais wa Afrika na kwamba rais atakayebainika kuwa anafuata misingi ya utawala bora na kuwawezesha raia wake kuwa na maisha mazuri basi atajinyakulia kitita cha dola za Marekani milioni 5 (zaidi ya shilingi bilioni 5 za Tanzania).

Lakini mshindi wa tuzo hiyo atakuwa pia akilipwa dola za Marekani 200, 000 (zaidi ya shilingi milioni 200) kila mwaka hadi ukomo wa maisha yake.

Binafsi niliposikia habari hizo nilijiuliza mambo mengi na baadaye nikaona si jambo jema kwa watawala wetu kupimwa uwezo wao wa kazi za kuwaongoza wananchi kwa mashindano na ahadi ya mamilioni ya pesa. Hapakuwa na haja hiyo na wala sioni kama umuhimu wa aina hiyo upo katika jamii zetu.

Hata hivyo, wakati naendelea kuwaza jambo hilo nikaikumbuka moja ya hotuba ya mtawala wa zamani wa Afrika Kusini P.W. Botha. Huyu ndiye mwasisi wa siasa za kibaguzi za rangi nchini humo aliyerejea kuzimu hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 90. Botha katika moja ya hotuba yake alipata kusema kuwa njia rahisi ya kuziteka akili za mtu mweusi basi mpe mwanamke wa Kizungu na hapo atakupa siri zote.

Lakini Botha hakuishia kusema hayo, katika hotuba yake hiyo na hata katika mazungumzo yake ya kawaida mara kwa mara alisema njia nyingine ya kuuteka ubongo wa mtu Mweusi mpe zawadi ya pesa na hapo atawajibika hata kama litakuwa suala la kumnyima usingizi.

Katika hilo, Botha hakumaanisha kuwa hakuna mwanadamu asiyependa pesa la hasha! Alichosema ni kuwa ni mazoea kwamba kwa mtu Mweusi hata jambo ambalo ni wajibu wake alifanye katika misingi fulani atapenda apewe ‘kitu kidogo’ ili aendelee kuwajibika. Kwamba anapopigwa ‘mjeledi’ wa pesa mambo hayaendi kombo.

Siku ile nilipoyafumbua macho yangu na kusoma habari kwamba kuna tuzo kwa ajili ya viongozi watakaoonekana kufuata utawala bora, nilipata mshangao kwamba iweje leo hii kuibuke na kitu kama hicho kwa watawala wetu.

Je, urais sasa ni kama mashindano ya Miss World ambako warembo hujiandaa kuanzia ngazi za chini lengo likiwa ni kuibuka kinara kwa wengine? Au urais wa Afrika umekuwa kama michuano ya Klabu Bingwa Afrika?

Kwa ufahamu wangu, viongozi wengi barani Afrika wameingia madarakani kwa kupigiwa kura za ndiyo na wananchi. Hawakuvamia Ikulu na kwa maana hiyo kulikuwa na maandalizi ya uchaguzi kwa kampeni za kuwania nafasi hiyo, kampeni ambazo bila shaka ziliambatana na ahadi juu ya nini watawafanyia raia wao pindi watakapopata ridhaa ya kutawala.

Leo hii, linaibuka la kuibuka kwamba marais wapimwe utendaji wao na kisha wapewe pesa kama zawadi. Huku ni kupotoka! Hawa wamekuwa watoto kwamba hawaendi kuoga hadi wapewe ahadi ya peremende? Wamekuwa watumwa kwamba hawawezi kufanya kazi hadi wachapwe na mijeledi kwenye migongo yao?

Huyu Mo Ibrahim ambaye pia ni mwanzilishi wa Kampuni ya Simu za mkononi ya Celtel kama kweli ana nia ya kuwasaidia watu wake ndani ya Afrika angeanzia nchini mwake alikozaliwa huko Sudan ambako hali si shwari katika Darfur. Angeanzia huko kama Waingereza wanavyoamini kuwa charity starts at home.

Nionavyo mimi, zawadi ya pesa kwa marais haiwezi kuijenga Afrika hata siku moja. Huo ndio mtazamo wangu na hicho ndicho ninachokiamini. Fisadi ni fisadi tu na hawezi kubadilika eti kwa sababu kaona pesa mbele yake. Kiongozi mwenye nia ya dhati huzaliwa na moyo wa aina hiyo na hujipanga kuwatumikia watu wake kwa haki hata kama itamlazimu kulala sehemu isiyo ya kifahari.

Ninachokiona ni kuudhalilisha utu kwa kigezo cha pesa. Kwamba kinachoonekana hapa si changamoto kama baadhi ya watu wanavyojaribu kuamini bali ni udhalilishaji kwa wakuu wa Afrika.

Kama nilivyodokeza hapo juu kuwa kigezo cha pesa kisiwe hoja ya msingi kuwapima watawala wetu. Mtu mwadilifu aliyepewa dhamana ya utawala wa nchi anatarajiwa kuwa mwenye kuumia na umaskini wa watu, mwadilifu sharti asilale usingizi pale anapoona raia wake wanakufa kwa magonjwa au njaa.

Hali kadhalika mwadilifu anapaswa kutokuwa mwenye makuu kwa kujinufaisha yeye wakati raia wake wakikosa elimu na huduma nyingine muhimu za jamii. Lakini katika hili, mwadifu pia ni yule ambaye atafanya na kutimiza majukumu yake pasipo kuwekewa mfuko wa mamilioni ya dola za Marekani mbele yake. Huyu ndiye anayetufaa!

Wenye kuandaa utaratibu huo wamepanga zawadi hizo kwa hao watakaoonekana kuwa watawala bora lakini je, na hao marais wazandiki na wadhalimu watapewa adhabu na nani? Bila shaka kuna mahala mpango huu utakwenda upogo.

Hivi kweli palikuwa na umuhimu wa kuanzisha tuzo hizi kwa wakati huu? Waandaaji hawakuona kuwa upo umuhimu wa kuwajengea mazingira mazuri raia wa kawaida kabisa ambao wamekuwa wakipata wakati mgumu kukabiliana na maisha ya kila siku?

Au tuseme kwamba yale yaliyopatwa kunenwa na Manabii kwamba mwenye nacho huongezewa yanaendelea kutimia? Rais wa nchi awaye yote anapostaafu hupewa mafao yanayomwezesha kuwa na maisha bora kwa kipindi kirefu lakini si mwananchi wa kawaida.

I wapi basi mipango ya kuwakomboa Waafrika kama mambo yenyewe ni haya? Zumari la kuwakataza hao wanaojifanya kuwa wanaidai Afrika madeni makubwa mbona halipigwi tena? Badala yake twaibuka na mambo ambayo kwa mtazamo binafsi hauna jema katika maendeleo ya Afrika zaidi ya kuwadhalilisha watawala wetu.

Sina hakika na akiba ya Mo Ibrahim katika akaunti zake za benki, lakini kama nilingelijua ningelimshauri jambo moja nalo ni kujenga shule za aina mbalimbali ndani ya bara hilo ili kufuta ujinga kwa mamilioni ya watu barani humo.

Lakini pia angeweza kujenga misingi ya kuwainua Waafrika moja kwa moja kwa kuanzisha kampuni ambazo zitatoa ajira kama alivyofanikiwa katika Celtel ambayo kwa sasa imeuzwa kwa wawekezaji wa Kuwait. Hili la kuwashindanisha wakuu wetu wa nchi kwa ahadi ya pesa kamwe sikubaliano nalo. Naomba kutofautiana!

munyuku@gmail.com

Tunahitaji kina Mwamnyenyelwa watatu tu

na innocent munyuku

KAMA kuna taarifa iliyonifurahisha katika mwaka huu wa 2006, basi hii ya Watanzania kugoma kuhutubia kwa lugha ya Kiingereza huko Nairobi nchini Kenya imenikuna zaidi.

Niliposoma kwenye magazeti na mitandao mingine ya habari kwenye intaneti juu ya habari hiyo nilivutiwa mno kiasi cha kunilazimu nisake nafasi ya kuwapa pongezi Watanzania waliodiriki kuitetea lugha yao wakiwa ughaibuni.

Bila shaka msimamo wa aina hiyo uliotolewa na Watanzania hao kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Vijana wa Afrika umewafurahisha pia na raia wa nchi hii. Wenzetu hao waliweka msimamo kwamba hawatahutubia kwa lugha nyingine zaidi ya Kiswahili katika mkusanyiko huo wa zaidi ya vijana 100 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Katika mkutano huo, waandaaji walipanga uendeshwe kwa Kifaransa au Kiingereza jambo ambalo wajumbe kutoka Tanzania hawakukubaliana nalo.

Aliyeanza kuwashtua washiriki wengine ni Hassan Bumbuli ambaye aliweka wazi msimamo wake katika utambulisho kuwa hakuwa tayari kuitumia lugha ya Kifaransa au Kiingereza katika kutoa mada mkutanoni hapo.

Kwa heshima na taadhima, Bumbuli akawataka radhi wajumbe wengine na akaeleza kuwa kwa vile mkutano huo ni wa Pan Africans na pia unafanyika kwenye ardhi ya Afrika Mashariki ambako Kiswahili ni nyumbani kwake hakuona sababu ya msingi kutoa hoja zake kwa lugha nyingine tofauti na hiyo.

Naamini kwa dhati kuwa Bumbuli wakati anatoa msimamo wake huo alihitaji akili ya ziada kuweka hadharani kile anachoamini katika mtima wake. Kwamba uhodari aliouonyesha mbele ya hadhira ile ulitokana na uchungu na uzalendo wa kukiweka Kiswahili katika mstari wa mbele.

Gazeti la kila siku la Majira katika toleo lake la Novemba 3, 2006 lilimkariri Bumbuli akisema “Nitaomba mnisamehe kwani sitopenda kuzungumza Kiingereza wakati huu ni mkutano wa Waafrika na tayari kama Afrika tunayo lugha ambayo tunaitazamia kuwa ya pamoja ambayo ni Kiswahili.

“Sasa mimi nitazungumza Kiswahili na lazima niwaeleze kwamba nimesikitishwa sana na waandaaji wa mkutano huu kuchagua lugha mbili tena za Wazungu kuwa ndizo lugha za kujadili hisia zetu Waafrika.”

Kutokana na msimamo huo, waandaaji wakaahidi kumweka mkalimani lakini kwa sababu ambazo hazikusemwa, mkalimani huyo hakuwekwa. Inawezekana walidhani kuwa nguvu ya Bumbuli ingeyeyuka kama povu la sabuni kwenye upepo wa jangwani.

Ikaja zamu ya mwakilishi mwingine kutoka Tanzania. Huyu ni Dadi Kombo aliyetakiwa kutoa mada ya Ushiriki wa Vijana katika Siasa. Naye bila ajizi akaanza kutoa mada kwa Kiswahili na hata juhudi za kumtaka abadili lugha hazikuzaa matunda. Aliendelea kuteta kwa Kiswahili na hapo ikabidi mada yake iahirishwe.

Wakati wajumbe wakiendelea kutafakari msimamo huo, mjumbe mwingine wa Tanzania, Mgunga Mwa-Mnyenyelwa aliyetakiwa kutoa mada juu ya sanaa kwa vijana pia akasimama na kuwaeleza wajumbe wengine kuwa kamwe asingewasilisha mada yake kwa Kifaransa au Kiingereza na kwamba angetumia Kiswahili.

Mgunga akawauliza waandaaji kwamba iweje atumie lugha tofauti na Kiswahili wakati mkutano huo ni wa Waafrika? Akaongeza kuwa asingekuwa tayari kuungana na waandaji katika kukidharau Kiswahili.

“…Kwa nini tunadharau mambo yetu ya Kiafrika na kuthamini Wazungu? Kiswahili kina nguvu sana na ni lugha inayotumiwa na watu wengi sana katika ukanda huu wa Maziwa Makuu, tusipoipa thamani lugha yetu katika mambo kama haya je, tutaithamini wapi na lini?”

Kwa msumari huo wa Mwa-Mnyenyelwa, waandaaji hawakuwa na haja ya kupinga hoja ya Watanzania kutaka kutumia lugha yao ya Kiswahili katika mkutano huo na hapo ndipo wakalazimika kumweka mkalimani na mambo yakaenda sawia.

Sitasahau tukio hili lililofanywa na Watanzania hawa na kamwe sitafumba mdomo wangu au kuuzuia ulimi wangu kunena pongezi juu yao. Naam wanastahili pongezi kwa ushujaa wao tena wakiwa nje ya ardhi ya kuzaliwa.

Mpigania uhuru wa Afrika Kusini marehemu Steve Biko katika harakati zake dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi nchini humo alipata kusema kuwa kitendo cha kujitambua kuwa wewe ni Mwafrika tayari umeanza vita dhidi ya wadhalimu!

Biko ambaye mara nyingi alipenda kujitambulisha kuwa ni Bantu Steve Biko alikuwa na kauli nyingine za hamasa juu ya kujitambua na kupigania kilicho chako. Katika hili alikuwa wazi kutamka katika mikutano yake kuwa mtu Mweupe hakuna maana kwamba wewe ni bora kuliko Mweusi hali kadhalika kuwa Mweusi hakuhalalilishi kuwa duni mbele ya mtu Mweupe.

Mwa-Mnyenyelewa na kundi lake wamejiweka katika mstari wa kupigania kilicho chao na kwa hakika wanapaswa kuwa miongoni mwa Watanzania wa kuigwa katika kukitetea Kiswahili ndani na nje ya nchi. Kwamba usipothamini chako si rahisi mtu mwingine akithamini.

Tumejikana vya kutosha katika miaka mingi, tukisahau mema ya kwetu. Tumejipunja uhuru wa nafsi kwa siku tele zilizopita. Ingawa maelfu wangali wakikana vya kwao, huu uwe mwanzo au mwendelezo wa vita dhidi ya wanaotaka kufifisha mila na utamaduni wetu. Huu ni wakati wa kujitambua kwa dhati kabisa na kukana ulofa na utumwa wa akili wa kukumbatia kila kitu kutoka ughaibuni. Kiswahili ni chetu hivyo lazima tujenge umoja katika kukitetea na kuhakikisha kuwa lugha hii inapanuka.

Kilichofanywa na Watanzania jijini Nairobi ni kuwakumbusha baadhi ya Watanzania ambao binafsi nawaita waasi ambao kazi yao ni kuthamini kila kitu kutoka nje ya mipaka yao. Hawa ni wale waliosahau lugha yao, hawataki pia mavazi achilia mbali vyakula vyenye asili ya Kiafrika. Hawa wamejaa tele!

Nimekuwa shuhuda na msikivu makini wa vioja vya lugha mitaani. Utakuta mtu Mzungu anajaribu kuwasiliana na Mtanzania kwa lugha ya Kiswahili lakini ajabu ya Mungu ni kuwa Mweusi huyo badala ya kuzungumza Kiswahili atapinda na kumjibu Kiingereza. Kwa mtazamo wangu Mtanzania wa aina hii hana na tofauti na askari anayewaua wenzake katika mapambano vitani.

Vita ya kukitetea Kiswahili wasiachiwe kina Mgunga pekee, Watanzania wote tushiriki na bila shaka hata waasisi wa taifa hili wazima kwa wafu watakuwa na furaha kuona kuwa lugha yetu imewaunganisha Waafrika na hapo ndipo mshikamano na umoja wa kweli wa Afrika huru utakapokuwa na maana pana. Afrika moja lugha moja! Kila jambo linawezekana katika uso wa dunia, ni suala la kuthubutu.

Ndio maana nasema twahitaji kina Mwa-Mnyenyelwa, Bumbuli na Kombo wengine ili kufanikisha vita hii mbele yetu.

Lakini kwa upande mwingine huu ni mwanzo tu wa vita ngumu iliyo ndani ya damu ya Waafrika katika kujivunia mambo yao ya asili. Kwamba tukimaliza ya Kiswahili twende kwenye majina yetu ya asili. Badala ya Innocent tujiite Navali, badala ya Charles tujiite Nangomo, badala ya Alfred tujiite Nandule.

Tusione soni kujiita Tuhwachi na kamwe tusiyafumbie macho majina kama Andulile, Anyimike au Nkungu. Haya ni ya kwetu na tusitarajie kuwa kina Smith kutoka Uingereza watayatangaza majina haya. Wataendelea kuyaita ya kishenzi!

munyukubantu@hotmail.com
0754 471 920

Monday, November 06, 2006

Ni watani au ‘wachawi’ wa jadi?

Ni watani au ‘wachawi’ wa jadi?

na innocent munyuku

KWA miaka mingi sasa, unapozungumzia upinzani wa soka nchini Tanzania, mashabiki wengi wa mchezo huo hawasiti kuzitaja timu za Simba na Yanga kuwa zenye upinzani wa kweli. Hawaishii hapo watasema pia kuwa timu hizo zina utani wa jadi.

Wanasema hivyo kutokana na historia ya timu hizo kongwe nchini kwamba kila zinapokutana kama si mmoja kufungwa basi hutoka sare ya mabao ama suluhu na kuna wakati moja ya timu hulazimika kuweka mpira kwapani.

Kwa Simba na Yanga mambo kama hayo ni ya kawaida. Kwamba si ajabu kusikia moja ya timu kati ya hizo ikitangaza kutoingiza timu uwanjani kwa sababu fulani na kweli ikafanya hivyo au wakati mwingine huwa ni tishio na wenyewe hudai kuwa ni moja ya mbinu katika soka.

Timu hizo mbili kila zinapojiandaa kukutana katika mashindano mbalimba iwe Ligi Kuu au michuano ya kuwania vikombe vingine, mashabiki wa pande zote mbili huingia mchecheto wa hali ya juu lakini kubwa ni kwamba majigambo hutawala wakati huo wa maandalizi.

Hata hivyo, homa ya maandalizi ambayo mashabiki wa Simba na Yanga wanakuwa nayo huambukizwa pia wachezaji wa timu mbili kwani kwa wakati huo hata wachezaji wa timu hizo huwa kwenye wakati mgumu. Katika miaka ya hivi karibuni ambako kuna teknolojia ya simu za mikononi, wachezaji hao kunyang’anywa simu zao mikononi ni jambo la kawaida.

Wanaoendesha utaratibu huo ni viongozi wa timu hizo na kama si hao basi ni wanachama watiifu wa klabu hizo ambao kimsingi hawapingwi katika utekelezaji wa kazi zao. Lakini kinachofanyika hapa ni kulinda maslahi ya klabu isihujumiwe na mpinzani.

Ipo minong’ono pia kuwa kuna wakati fulani wachezaji hulazimika kulala makaburi au kupakwa dawa za jadi zitakazowasaidia kuwa imara uwanjani. Kwa ujumla wakati wa kuelekea mechi za Simba na Yanga kila jambo husemwa ili mradi kuwa katika porojo za maandalizi ya mechi.

Lakini jambo moja ambalo liko wazi ni kwamba kinachoangaliwa katika mechi ya Simba na Yanga ni kujijengea heshima kwa mashabiki wake. Hakuna anayekubali kuchekwa kwa kipigo uwanjani na hii ndio asili ya madoido yote hayo kabla ya mechi.

Hata zinapotoshana nguvu, mashabiki wa timu hizo hawakosi maneno kwenye ndimi zao. Watasema kila linaloonekana kuwa lafaa kuwa kejeli kwa wapinzani wao.

Mfano ni katika mechi ya Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga wanadai Simba walikuwa na ‘mzigo mzito’ wa ndumba kutoka Bagamoyo huku wapinzani wakisema kuwa ‘uchawi’ wa kipa wa Yanga, Ivo Mapunda wa kubadilisha viatu uliwapa nguvu dimbani.

Kabla ya mechi hiyo, gazeti la Daily News katika ukurasa wake wa nyuma lilikuwa na habari kwamba mechi hiyo iligubikwa na uchawi wa hali ya juu. Katika habari hiyo, kuna picha zinawaonyesha watu wawili ambao hawakujulikana ni wa timu ipi wakiwa katika jitihada za kufukia vitu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ninapoyaangalia mambo kama haya yakiendelea kufanyika katika uso wa dunia kwa karne hii huwa naduwaa. Lakini kuduwaa kwangu si kwamba sina jawabu la hasha! Jibu lipo, nalo ni ufahamu kuwa jamii yetu haitaki mabadiliko hata kwa wakati huu ambao hatuhahitaji kuamini masuala ya ndumba katika soka.

Nani alishaona ndumba zikitembea wakati au kabla ya mechi kati ya Manchester United na Machester City huko Uingereza? Au ni nani atasimama na kunena kwamba ameshaiona Liverpool na Arsenal zikishindania uchawi kabla ya mechi yao?

Ninachotaka kusema ni kwamba suala la uchawi katika soka halina maana kwa soka ya Tanzania leo hii. Huu si muda wa kurusha manyonya ya kuku au kutupa pembe za ng’ombe uwanjani. Wachezaji hawana budi kufuata mafundisho ya makocha na hakuna haja ya kuendekeza imani za kishirikina katika soka.

Kwa mtindo huu mwadhani akina Gaudence Mwaikimba au Emmanuel Gabriel wataweza kung’ara ughaibuni? Watatamba vipi wakati walishazoea kuamini kuwa pasipo ndumba mpira hauchezeki? Sisemi kwamba kwamba hawa wawili ndio vinara wa ndumba bali timu zao zimekuwa zikionyesha hali ya ushirikina kabla ya mechi.

Kama kuna kiongozi kati ya timu hizo atasema hahusiki na mambo kama hayo, mbona hajawahi kujitokeza na kulaani mambo kama hayo? Ukweli ni kwamba imani kama hizo zimejengwa ndani ya klabu hizi na bila shaka na zingine zilizojaa hapa nchini.

Huu uwe wakati wa kusema hapana kwa mambo kama hayo. Nyakati za kuamini kuwa shuti kali halitalenga golini eti kwa sababu milingoti imemwagiwa maji ya maiti zimepitwa na wakati. Tuwaachie makocha wafanye kazi zao na wachezaji wawajibike kwa kufuata maelekezo uwanjani.

Ninapoona watu wanapoteza pesa kwa ajili ya ushirikina wa kujipatia ushindi uwanjani huwa nabaki mdomo wazi kwa kuwaonea huruma wahusika na hapo ndipo ninapoona kuwa Simba na Yanga si watani wa jadi bali ni ‘wachawi’ wa jadi.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni suala la kukimbiana limeanza kutoweka tofauti na miaka ya nyuma kama ilivyokuwa Novemba 26 mwaka 1966 pale Yanga ilipoondoka uwanjani zikiwa zimesalia dakika tatu mpira uishe.

Katika mechi hiyo mchezaji Awadh Gessani aligoma kutoka nje licha ya kuamriwa na mwamuzi Jimmy Waldon baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Sunderland (Simba). Sunderland ilipewa ushindi wa mabao 2-0 huku nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’ akifungiwa na FAT kucheza soka kwa miezi 12.

Lakini pia katika mechi ya Machi 30, 1968 mchezo uliishiia katika dakika ya 28 baada ya mshambuliaji wa Sunderland, Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’ kumvamia mwamuzi Jumanne Salum. Yanga ilipewa ushindi.

Pia Machi 3, 1969 Sunderland haikutokea dimbani na hivyo kuipa ushindi Yanga huku Sunderland wakipigwa faini ya sh 500. Hata Machi 21 mwaka 1971, Sunderland iligoma kuendelea na mechi kunako dakika ya 70 kwa madai kuwa kipa wao John William Semainda aliumizwa. Mgomo kama huo ulitokea katika mechi ya Juni 18, 1972 wakati Yanga ikiongoza kwa bao 1-0 liliwekwa kimiani na Leonard Chitete.

Agosti 26 mwaka 1992, Yanga ilileta ‘jeuri’ kwa kutokubali kucheza na Simba kwa madai kuwa tayari ilishatwaa ubingwa. Mgomo waom huo uliwagharimu faini y ash 250,000

Hiyo ni mifano michache tu ya mambo ambayo timu hizo zimekuwa zikijihusisha nayo katika ulimwengu, masuala ambayo hayana mema kwa maslahi ya soka nchini.

Na ndio maana wakati mwingine nashawishika kusema kuwa Simba na Yanga ni makaburi ya wachezaji kutokana na vitendo vyao ambavyo havina misingi ya kuimarisha soka kwa wanasoka wake.

Lucy Kihwele: Akumbuka alivyopokwa taji Miss Tanzania 1994

Lucy Kihwele: Akumbuka alivyopokwa taji Miss Tanzania 1994

-Asema mimba waachiwe wenye ndoa
-Ahimiza elimu ya uzazi ngazi ya familia

na innocent munyuku

IJUMAA ya Oktoba 6 mwaka huu nainua simu kumjulia hali mwanamama ambaye kutokana na pilika za jiji la Dar es Salaam sijamtia machoni kwa miaka kadhaa. Huyu ni Lucy Kihwele ambaye kwa furaha ananieleza kuwa siku ya pili yake anatimiza miaka 11 ya ndoa yake na Beraldo.

Kabla ya ndoa hiyo iliyofungwa Oktoba 7, mwaka 1995 katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, mwanamama huyo alijulikana kama Lucy Tabasamu Ngongoseke. Mrembo aliyepamba kurasa za magazeti mbalimbali ndani na nje ya nchi kutokana na ushiriki wake katika medani ya urembo.

Ni mmoja wa warembo walioshiriki mashindano ya Miss Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1994 tangu yapigwe marufuku na Serikali katika miaka ya 1960 kwa maelezo kuwa hayakuwa na mema katika kuendeleza mila ya Mtanzania.

Kujiamini kwake na namna alivyokuwa amejiandaa katika mashindano hayo mwaka huo kuliashiria mengi katika kambi yake na kubwa ni kwamba angeweza kuibuka na taji la Miss Tanzania. Lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo kwani aliishia nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikienda kwa Aina Maeda.

Hadi hii leo Lucy anasema ushindi wa Aina ulikuwa na kigugumizi kwani aliingia katika kinyang’anyiro hicho zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya fainali. “Nashukuru kwamba nilipata nafasi ya pili lakini mimi na wenzangu tulishangaa mtu anakuja kambini siku tatu kabla ya mashindano na anakuwa mshindi..kwa nini hakupitia hatua tulizopitia sisi, nadhani haikuwa sahihi kwa kweli,” anasema Lucy.

Pamoja na uchungu huo Lucy anabaki kuwa mmoja wa warembo wa Tanzania ambaye hadi sasa anasikika katika huduma za jamii kwa nafasi yake ya Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Multi Choice alikoajiriwa tangu Agosti mwaka 1997 akitokea Dtv ambako alifanya kazi ya utangazaji, mauzo na utawala kwa nyakati tofauti.

Kuhusu rushwa ya ngono katika mashindano ya urembo nchini, Lucy anasema kuwa mambo kama hayo yanakuwa hayana ushahidi na kwamba kama yapo wanaotakiwa kuyakemea ni washiriki wenyewe.

“Huwezi kupata ushahidi, mimi nasikia kwamba yapo lakini siwezi kuthibitisha na nikizungumzia kwa upande wetu sisi hapakuwa na mambo kama hayo,” anasema.

Kuhusu kuboronga kwa warembo wa Tanzania kwenye mashindano ya Miss World, Lucy anasema lazima hatua za makusudi zichukuliwe hasa katika kuangalia warembo wenye vipaji.

“Tusikate tamaa lakini ukweli ni kwamba tuwapeleke wasichana wenye vipaji na watafute vigezo vya kimataifa. Mrembo awe na vipaji walau viwili na hapa ieleweke kuwa kipaji si kuimba na kucheza muziki pekee.

“Lakini pia kuna tatizo jingine katika safari ya kwenda mashindanoni, sisi watazamaji tumekuwa tunawafanya hawa watoto wayumbe kwa kuwalazimisha wazungumze Kiingereza jukwaani.

“Tunawasukuma waseme Kiingereza hata kama hawakijui kwa upana zaidi, msichana akizungumza Kiswahili anachekwa…hii inashangaza sana.”

Pamoja na uelewa wake wa masuala ya urembo, Lucy mama wa watoto wawili anakerwa na mabinti wanaoshika mimba huku wakiendelea na masomo yao.

“Hili jambo linanikera sana na kwa hakika linanisumbua moyoni. Huwa najiuliza inakuwaje msichana apate mimba wakati akijua kuwa ana masomo yanamkabili?

“Na mpango kwamba wakishapata mimba waondoke shuleni na kisha warejee na kuendelea na masomo ni sawa na kumwaga petroli kwenye moto. Watazoea na wasichana wengine wataona kuwa ni jambo la kawaida.

“Unaporuhusu jambo la aina hiyo ni wazi kuwa unatetea pia maambukizi ya ukimwi. Mimi nawashauri hawa watoto wachague jambo moja shule au mimba na wajue kuwa mimba wawaachie wenye ndoa.”

Anasema kwa vile wavulana wanaohusika na mimba hizo huendelea na shughuli zao na wengi wao pasipo kubughudhiwa, hilo linaweza kuwa funzo kwa wasichana kuacha ngono zembe kwani ni wao ndio wanaokosa mtiririko mzuri wa masomo yao.

“Kwa mfano mvulana aliyempa mimba binti anaendelea na masomo na msichana analea mimba na baadaye mtoto sasa hapo kwa akili ya kawaida binti lazima ajifunze kuwa suala la kukimbilia maisha ya aina hiyo lazima liepukwe,” anasema Lucy.

Lakini kwa upande mwingine Lucy anaeleza kuwa wazazi wanastahili lawama kwa mimba za utotoni pamoja na maambuziki ya magonjwa kwa watoto. Kwamba wapo wazazi na walezi ambao hawajishughulishi na utoaji wa elimu ya uzazi kwa mabinti zao.

“Si jambo geni, wapo kina mama ambao hadi sasa hawako tayari kumweleza binti hali ya maungo yake na jinsi yanavyofanya kazi, wanaona aibu. Sasa aibu hiyo ndiyo inayosababisha watumbukie katika mimba zisizotarajiwa.

“Mabinti wengi wanarubuniwa na wanapojaribu wanajikuta wameshanasa kwa sababu hawakuwa na elimu ya uzazi. Hawajui jinsi ya kujikinga,” anasema.

Pamoja na hilo amewaasa wasichana kutokubali kuingia katika mtego wa wanaume wanaotaka wawape mimba kabla ya ndoa. “Kama anakupenda kwa dhati atakusubiri na ukiona mtu anakimbilia uzazi kwamba jua kuwa hana mapenzi ya kweli.

“Binafsi nilianza uhusiano na Beraldo tangu mwaka 1984 tukafunga pingu za maisha mwaka 1995, miaka 11 baadaye. Wazazi na ndugu wakatarajia kuwa baada ya ndoa tu tungeanza kuzaa, nikawaambia kuwa sijafuata kuzaa bali mapenzi.”

Lucy alizaliwa miaka 34 iliyopita huko Magu mkoani Mwanza na alipata elimu yake ya msingi Shule ya Msingi Kinondoni na Lyalamo iliyoko Tosamaganga, Iringa. Alisoma shule ya Sekondari ya Wasichana ya Masasi na Jangwani na mwaka 1987 alikwenda nchini Marekani kwa elimu ya juu.

Ana watoto wawili Regina mwenye umri wa miaka minane na Reginald mwenye umri wa miaka minne.

Mbali na mapenzi makubwa kwa familia yake, Lucy ni mpenzi wa kuimba, kupika, safari na kupumzisha mwili wake katika pwani ya bahari au ziwa.

“Lakini katika kuimba huwa napenda kufanya hivyo nikiwa bafuni,” anasema na kisha kuangua kicheko kinachohitimisha mazungumzo baina yangu na mwanamama huyo ambaye ni mcheshi na sura ya tabasamu kwa muda mrefu.

epuka utumwa wa akili: November 2006

Manji: Sikuingia Yanga kujitangaza

Manji: Sikuingia Yanga kujitangaza

na innocent munyuku

MAPEMA Juni mwaka huu, Klabu ya Yanga iliingia katika moja ya hatua ya maendeleo baada ya kupata ufadhili kutoka kwa Kampuni ya Gaming Management Tanzania Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara Yusuf Manji.

Ilikuwa hatua muhimu kwa Yanga kwani ni katika kipindi hicho, wanachama wa klabu hiyo walikuwa wakisigana na hivyo kuipa wakati mgumu timu ambayo kwa muda huo ilihitaji umoja ili ifanye vema katika Ligi Kuu Tanzania Bara na hivyo ndivyo ilivyokuwa, Yanga ni bingwa mwaka huu.

Mara baada ya kusaini mkataba huo, pande zilizokuwa zikitofautiana, Yanga Kampuni, Yanga Asili na Yanga Academia zikakubali pia kumaliza tofauti zao kwa maslahi ya Yanga na wanachama wengine.

Hakuna shaka kwamba ni Manji ndiye aliyeshinikiza kumalizwa kwa tofauti zilizokuwapo na akajitolea kuifadhili ziara ya wanachama wa Yanga chini ya Yusuf Mzimba katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kufuta makundi na kambi zilizokuwa katika ugomvi.

Alipogusa klabu hiyo, jina la Manji licha ya kuwa lilishakuwa maarufu kabla, wapenzi wa klabu hiyo walimwongezea umaarufu kwa kumtukuza na kumwona kuwa mwokozi wa klabu hiyo.

Katika mahojiano maalumu na RAI mwishoni mwa wiki iliyopita, Manji anasema hakupenda kutukuzwa kwa kiasi kikubwa kama walivyofanya mashabiki na baadhi ya wanachama wa Yanga.

“Jina langu lilianza kupewa sifa kubwa kiasi kwamba sikupenda. Yanga walinichukulia kama mwanga na hali hii ilinitisha sana,” anasema Manji na kisha kuongeza:

“Yanga ilikuwapo tangu zamani na mimi lengo langu lilikuwa very simple, nalo ni vijana wawe nje na mambo yanayowaathiri kama vile ukimwi na dawa za kulevya.

“Nilianza kuwa na wazo hili tangu wakati wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa wabunge na rais mwaka jana. Kule Kigamboni nikawaahidi vijana kuwa nitawainua katika mambo mengi ikiwamo michezo,” anaeleza Manji ambaye katika uchaguzi huo alikuwa akiwania kupitishwa kuwania kiti cha ubunge.

“Kwa hiyo nikaona nini vijana wanapenda, nikagundua kuwa ni soka. Sasa nikasema kwa vile ni soka basi nitumie mwanya huo kuwatoa mitaani. Na njia mojawapo ni kuwainua wachezaji wa Yanga wawe bora ili vijana wengine waone fahari kucheza soka.

“Ulaya na sehemu nyingine duniani wana role models…mtoto anakua na kutamani maisha ya mtu fulani aliye juu katika jamii. Kwa hawa wa Yanga wakifanikiwa kuwa hapo ni wazi kuwa watakuwa walimu wazuri katika kuielimisha jamii.

“Beckham au Jay Z hawezi kutoka Ulaya kuja kutufundisha maadili hapa kwetu, tunatakiwa sisi wenyewe tufanye kazi hiyo.”

Anasema kuwa kutokana na kutambua hilo ndio maana akaona ni busara zaidi kuwajengea wachezaji mazingira mazuri kimapato. “Huwezi kuwa mchezaji bora wakati huna kitu…na idea yangu hapa ni kuwa na Ronaldo wetu.

“Kutokana na mawazo kama hayo ndio maana nasema na nataka nieleweke kuwa sikuingia Yanga kutafuta umaarufu bali kutimiza ahadi yangu kwa watoto niliyoitoa Kigamboni.

“Wapo walioifanya Yanga kuwa sehemu ya kupata umaarufu na pesa pia…lakini mimi si mmoja wao.”

Hata hivyo, Manji anasema kuwa pamoja na nia nzuri aliyo nayo, bado anahitaji ushirikiano wa hali ya juu na wadau wengine na kwamba lazima pesa anazotoa ziende kwa walengwa ambao ni wachezaji.

“Ninachoamini ni kuwa huwezi kuwa na timu bora kama huna wachezaji wazuri klabuni. Hawa wachezaji wakiwa na confidence uwanjani lazima wafanye vizuri na ndio maana ubingwa umekuja mapema.”

Kuhusu Yanga kuwa kioo cha jamii, Manji anaeleza kuwa mikakati inasukwa ili wachezaji siku zijazo waendeshe darasa la elimu kuhusu ukimwi au dawa za kulevya kwa vijana wenzao.

“Watapita (wachezaji) kila mahala kusema kwamba jamani hiki hakifai fuateni njia hii au fanyeni hivi hawa watakuwa sasa community hope.

“Lakini niwaambie kitu kingine kwamba Yanga has great future na ndio maana sikupenda kuona migongano ndani yake. Lazima tujadili tofauti zetu na sana sana tuwajali wachezaji kwa sababu hawa ndio kiini cha maendeleo.

“Ifike wakati mchezaji awe na heshima mtaani na si mtu wa kudharauliwa kwa sababu kama wataendelea hivi hakuna jema mbele yao na mbele ya Yanga pia.”

Lakini kuna jambo moja ambalo Manji katika mazungumzo yake hawezi kuliacha bila msisitizo nalo ni hisa kwa Yanga. Anasema lazima ununuzi wa hisa upewe kipaumbele kwani watu wengi au kampuni nyingi duniani zimefanikiwa kwa mtindo huo.

Kwamba ifike siku Yanga ijiendeshe kwa utajiri wake badala ya kumtegemea mtu mmoja au kampuni fulani.

“Leo hii tunawekeza na si jambo la busara kutegemea matunda leo, yafaa kuwa na subira lakini subira yenye matumaini ya maendeleo. Na lazima Yanga wajali umuhimu wa hisa.”

Katika mpango wa kuipa neema Yanga, Manji anasema kuwa utaratibu unaandaliwa ili kuanza kuuza fulana na kofia zenye majina ya wachezaji wa Yanga ili kutunisha mfuko wa klabu.

Anasema mapato ya mlangoni hayatoshi kuijenga klabu hiyo na kwamba mauzo ya fulana na mipango ifananayo na hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuijenga Yanga imara.

0754 471 920

Vicencia Shule:Kutoka kuuza baa hadi uhadhiri Chuo Kikuu

-Asema wasomi wanalamba miguu ya wafadhili
-Atetea uvaaji wa ‘vimini’

na innocent munyuku

AKIWA na umri wa miaka 24 tu tayari alishakuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani akifundisha sanaa. Huyo ni Vicencia Shule ambaye Oktoba 14 mwaka huu alifanya mahojiano maalumu na RAI na kueleza mambo mbalimbali yanayohusu kumwezesha mwanamke kifikra.

Alipojiunga na masomo ya Chuo Kikuu Septemba mwaka 1999 akitokea Shule ya Mkwawa alishiriki kikamilifu katika harakati za kuwatetea wanawake katika mradi uliopewa jina la TUSEME chini ya Profesa Amandina Lihamba. Kuanzishwa kwa mradi kulitokana na hali ya jamii katika kuwakandamiza wanawake katika nyanja mbalimbali.

Kutokana na ukandamizwaji huo, idadi ya wasichana waliokuwa wakipata fursa ya elimu ilikuwa ndogo na waliobahatika kupata elimu ya sekondari wengi wao walishindwa kujiunga na vyuo vikuu kutokana na mfumo mbovu uliowafanya wasipate mwanya wa kufika huko.

Vicensia ambaye ni mchangamfu na mwenye kujiamini katika mazungumzo yake anasema mradi wa TUSEME ulimsaidia yeye binafsi kwani alipata nafasi ya kuendelea kujitambua.

“Lakini hatukuishia kupata elimu na kukaa nayo, baada ya kufundishwa uwezeshaji tukaenda katika shule mbalimbali na walengwa hasa ni watoto wa kike, lengo la huu mradi ni kumweka mtoto wa kike ajitambue,” anasema Vicensia.

Mradi huo ulioanza mwaka 1996 ulianza kuonyesha cheche zake katika shule za sekondari za wasichana za Kilakala, Songea, Korogwe, Msalato, Iringa na shule mchanganyiko ya Bagamoyo na Ruvu.

“Nathubutu kukueleza kuwa wasichana wengi ambao walifikiwa katika mradi huu ni wenye kujiamini katika jamii, hawako legelege kama wengine kwa sababu walifundishwa kujiamini na wana msimamo,” anaeleza.

Tangu wakati huo amekuwa akisimama msitari wa mbele kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto na kuvunja ukuta uliowatenga na haki katika jamii.

Je, katika umri huo mdogo anawezaje kuhimili darasa ambalo pia lina watu wazima waliomzidi umri? Anasema kimsingi hajawahi kujenga hofu kwamba yuko mbele ya watu wazima au wanaume.

“Sijawahi kutishwa kwa sababu naamini ninachofundisha ndio moja ya msingi wao katika elimu na kama kuna wanaonidharau sijawahi pia kuwaona.

Pamoja na hilo, Vicensia anakerwa na tabia ya baadhi ya wasomi ambao kwa sasa akili zao zimehamia tumboni badala ya kichwani.

“Sasa hivi walio wengi wanafikiria kutoka tumboni, wanaogopa kuikosoa Serikali na hii imetokana na ukweli kwamba wameathiriwa na donors (wafadhili).

“Wanaogopa kukosoa kwa sababu ya hofu…hawa wanaogopa kama watakosoa watakosa pesa za wafadhili kutoka nje, miradi mbalimbali inapita tu bila kufanyiwa utafiti.

“Kinachoendelea hapa ni kuwalamba miguu wanaokupa pesa za kuendelea na miradi, ndio maana sasa wako kimya hawasemi kabisa.”

Anapozungumza uongozi wa awamu ya nne katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Vicensia anasema Rais Jakaya Kikwete amejitahidi kuwafanya watu warudishe imani kwa Serikali lakini hana budi kuwa makini zaidi na katika hilo asiwaamini sana watendaji wake.

“Sisemi kwamba Serikali zilizopita zilikuwa mbovu hapana. Ninachosema ni kuwa Kikwete katupa kauli wananchi. Sasa hivi mwananchi anasikika tofauti na huko nyuma.

“Lakini safari yake ni ndefu, aendelee kurudisha imani kwa wananchi na si kwa hotuba zenye maneno mazuri bali kwa vitendo. Tumeona moja ya tume yake inafanya kazi, wahusika wamefikishwa mbele ya sheria na kesi inaendelea. Miaka ya nyuma ilifika mahala watu wakasema hatutaki tena tume za uchunguzi,” anasema na kuongeza:

“Suala la umeme nalo si jambo ambalo linataka siasa kwa sababu athari ni kubwa kwa taifa. Ni wazi kuwa waliotangulia walikosea. Hawa planners walikosea na hawataki kukubali, lakini mimi naona kukubali kosa ni uungwana kuliko kuwa mkaidi.

“Haya watasema kuwa vyanzo vya maji viliharibiwa, fine! Sasa wao walikuwa wapi wakati mambo yakiharibika? Kwa mtindo huu tunatingisha uchumi.”

Anapozungumzia suala la maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, Vicensia anasema pamoja na ukweli kwamba ugonjwa huo ni hatari bado upo umuhimu kwa baadhi ya taasisi kubadilika katika utoaji wa elimu.

“Nimesikia wengine wakisema eti mbio za mwenge zinaeneza ukimwi sasa hapo mimi hushangaa. Hivi kweli mtu atakaa mwaka mzima bila kufanya ngono akisubiri mbio za mwenge? Kwa kweli tusidanganyane,” anasema.

Hata hivyo, anasema kitendo cha baadhi ya viongozi wa dini kukataza matumizi ya kondomu katika mapenzi nacho ni sawa na uuaji. “Wannatukataza tusitumie kondomu, tukifa sadaka zitatoka wapi?

“Njia hapa ni kuangalia jinsi ya kuwaokoa waumini na si kuzuia matumizi ya kondomu kwa sababu kanisa linahitaji watu ili lijiendeshe. Mimi ni Mkatoliki na ninavyojua misaada kutoka Roma haipo na kwa maana hiyo tunajitegemea,” anasema.

Vicensia ni binti mwenye misimamo ambayo lazima umeze mate ndipo uweze kumwelewa. Wakati mwingine unaweza kudhani anatania lakini binafsi husisitiza kuwa anamaanisha anachosema. Mfano ni msimamo wake kuhusu mavazi.

Anasema hakuna mtu atakayeweza kumfunga minyororo ya akili kwamba achague nguo fulani ya kuvaa. Atafanya hivyo kama ataona inafaa kwa wakati huo lakini si kwenda na upepo usiojulikana umetokea wapi.

“Wanasema wasichana wanatembea nusu uchi, kwani sheria ya inasemaje? Kuvaa min skirt si kosa kwa mujibu wa sheria. Itakuwa kosa kama mtu katembea uchi wa mnyama kwa maana bila nguo.

“Kama wanasema tunawatamisha ni sawa lakini hata sisi tunatamani pia. Ukipita mjini mbona wanaume wanatembea vifua wazi? Msimamo kwamba wanawake ndio wazibe miili yao na wanaume watembee vifua wazi huu ni udhalilishaji.

“Hapa wasitake kuchanganya dini na masuala ya kawaida. Imani za dini waachiwe masheikh na mapadri. Mimi kwa mfano siku nikivaa kimini halafu wanishambulie hakika nitapigana hadi kifo, sitakubali.

“Kama wanasema tunawatamanisha itafika siku watazoea kuona mapaja na akili zao zitahamia kwa wanawake waliovaa hijab.”

Akizungumzia kuhusu wanenguaji wa kike katika bendi za muziki wa dansi wanaovaa nguo zinazoonyesha sehemu kubwa ya miili yao huku wanamuziki wa kiume wakivaa suti, Vicensia anasema jambo hili linapaswa liangaliwe kwa upana zaidi.

“Je, watazamaji walishagoma kuangalia dansi kwa sababu ya mavazi? Waajiri waulizwe na hawa mabinti waulizwe na Serikali pia iseme kama kuna sheria inazuia jambo hili. Mawaziri wengi wameshawahi kuangalia maonyesho ya aina hiyo, je, wao wametoa msimamo gani?”

Anasema suala la mavazi wakati mwingine huendana na miiko ya kazi ya mhusika kama ilivyo kwa baadhi ya ofisi ambazo lazima uvae nguo fupi kama hukubali basi unaondoka.

“Nimezaliwa huru na lazima niwe huru, nivae kitu ninachokipenda na ndio maana kama mwanamume nampenda hata kama nimekutana naye kwa mara ya kwanza nitamweleza. Wanawake lazima tuwe wazi kusema kilicho moyoni manake hata sisi tunatamani kama walivyo wanaume.”

Vicensia ambaye katika miaka ya nyuma aliwahi kuuza baa yao ya Safari iliyoko Maili Sita nje kidogo ya mji wa Moshi, alizaliwa Machi 14, 1978 ni kitinda mimba katika familia ya watoto wanane. Sita wa kike na wawili wavulana.

Alilazimika kuuza baa kama mchango wake katika familia ili kutunisha pesa zake za masomo na mahitaji mengine ya msingi.

“Tusiibeze kazi hii ya baa kwa sababu watu wengi inawasaidia kutunza familia na mimi nimefanya kumsaidia mama kufanya hesabu na kuwasimamia wafanyakazi wengine.”

Alisoma Shule ya Msingi Kilimanjaro mwaka 1985 hadi 1991 na kisha Shule ya Sekondari Mawenzi mwaka 1992-1995 kabla ya kujiunga Mkwawa mwaka 1996-1998. Alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuchukua shahada ya kwanza ya sanaa. Alimaliza Shahada ya Uzamili mwaka 2004 miaka miwili tangu aajiriwe katika nafasi ya uhadhiri chuoni hapo.

Vipi kuhusu ndoa? “Hilo ni jambo ambalo halipo kwenye akili yangu kabisa acha nikae kwanza na wala sijali nitakaa kwa muda gani.”